Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Sikaonga akiwapatia vipeperushi wananchi waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa afya pamoja na kuchangia damu wakati wanawake wa Taasisi hiyo wakiadhimisha siku ya wanawake duniani leo katika viwanja vya JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mainda Hamu akimpima shinikizo la damu (BP) mwananchi aliyejitokeza kupima afya wakati wanawake wa Taasisi hiyo wakiadhimisha siku ya wanawake duniani leo katika viwanja vya JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
07/03/2026 Zaidi ya Wananchi 100 wamejitokeza kushiriki zoezi la uchangiaji wa damu pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya moyo lililofanyika leo katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Upanga na Tawi la JKCI lililopo katika soko kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8 ambapo wanawake wa JKCI wamejitolea kusaidia jamii na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Kupitia zoezi hilo JKCI imeweza kukusanya uniti 21 za damu ambazo zitasaidia kuokoa maisha ya watoto watakaofanyiwa upasuaji wa moyo katika taasisi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Naizihijwa Majani alisema wamefanya zoezi hilo kama sehemu ya kurudisha kwa jamii kwani wao pia wanajukumu la kusaidia jamii na kuokoa maisha kwa kuchangia damu.
Dkt. Naizihijwa ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi aliwataka wananchi kulinda afya zao kwa kuzingatia lishe bora na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo.
“Ni muhimu jamii itambue umuhimu wa lishe bora, kufanya mazoezi na kufanya uchunguzi wa mapema ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwemo vifo vya ghafla”, aliongeza Dkt. Naizihijwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wa JKCI, Afisa Muuguzi Sr. Theresia Marombe alisema chama hicho kina jukumu la kusaidia jamii kwa kusogeza huduma za moyo karibu na wananchi bila malipo.
“Tumeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa huduma za uchunguzi wa moyo, uchangiaji wa damu na kutoa elimu elimu ya lishe ili kulinda jamii na kupunguza hatari ya vifo vya ghafla”, alisema Sr. Theresia.
Nao wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za afya ya mioyo yao pamoja na wasaidia watoto watakaofanyiwa upasuaji wa moyo kwa kuchangia damu.
“Namshukuru Mungu leo nimeweza kujua hali yangu ya kiafya bila malipo yoyote, kwani mara nyingi nimeshindwa kufanya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kutokuwa na fedha za kulipia gharama hizo”, alisema Praygod Ngowi mkazi wa Kimara.
“Baada ya kusikia kuna uhitaji wa damu kwa watoto wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji, nimechukua jukumu la kuchangia damu. Naomba wengine pia wajitokeze kusaidia kuokoa maisha ya watoto”, alisema Adeline Berchimance mkazi wa Mbezi.
Zoezi hilo la upimaji wa magonjwa ya moyo pamoja na kuchangia damu linaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za afya, wananchi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana, maisha yanaokolewa na afya ya jamii inaimarishwa.





