Benki ya KCB Bank Tanzania imeendelea kuonesha mchango wake katika kukuza maendeleo ya kifedha na biashara ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kushiriki katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha.
Mkutano huo uliofanyika Machi 7, 2026 ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo, ukilenga kujadili masuala muhimu ya kiuchumi yanayochochea ushirikiano wa kikanda.
Akiongoza ujumbe wa benki hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa KCB Bank Tanzania, Cosmas Kimario, alishiriki majadiliano yaliyojikita katika maendeleo ya fedha za kidijitali, ukuaji wa masoko ya mitaji pamoja na mbinu za kurahisisha biashara kati ya nchi wanachama wa EAC.
Ushiriki wa benki hiyo unaonesha dhamira ya sekta ya fedha katika kusaidia juhudi za kikanda zinazolenga kuongeza ufanisi wa mifumo ya kifedha na kuwezesha wafanyabiashara kunufaika na fursa za soko la pamoja.
Katika hatua nyingine, uzinduzi wa mfumo wa “EAC Customs Bond” umetajwa kuwa hatua muhimu itakayochangia kuimarisha biashara ya mipakani kwa kurahisisha taratibu za usafirishaji wa bidhaa na kupunguza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Kupitia ushiriki huo, KCB Bank Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake kama mshirika muhimu katika juhudi za kukuza uchumi wa kikanda na kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya kifedha na biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.




