Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) limetangaza kuwa maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Haki za Mtumiaji Duniani kwa mwaka 2026 yatafanyika jijini Tanga tarehe 15 Machi 2026, yakilenga kuhamasisha ulinzi wa haki, usalama na ustawi wa watumiaji wa bidhaa na huduma nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Machi 10, 2026, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, D.G. Daudi, amesema maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu haki na wajibu wao kama watumiaji wa huduma mbalimbali zinazodhibitiwa.
Aidha Daudi amesema kuwa, maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Bidhaa Salama, Watumiaji Wenye Kujiamini,” inayolenga kuhimiza upatikanaji wa bidhaa na huduma salama zinazokidhi viwango vya ubora ili kuwajengea watumiaji uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Amesema watumiaji wenye kujiamini ni wale wanaopata bidhaa na huduma salama, wanaofahamu haki na wajibu wao pamoja na kuwa na uwezo wa kuhoji ubora wa huduma wanazotumia.
Daudi ameeleza kuwa katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, TCF imeandaa shughuli mbalimbali za utoaji elimu kwa umma zitakazoanza Machi 10 hadi 15, 2026 kupitia vipindi vya vyombo vya habari na semina kwa makundi tofauti ya watumiaji.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yataweka msisitizo katika usalama wa huduma na bidhaa katika sekta mbalimbali zinazodhibitiwa, ikiwemo huduma za nishati na maji, usafiri wa anga, usafiri wa nchi kavu pamoja na huduma za mawasiliano.
Kwa upande wake, jukwaa hilo limewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo ili kupata elimu kuhusu haki zao na kutumia mifumo iliyopo kuwasilisha maoni au malalamiko kuhusu huduma wanazopokea.
Wananchi wa jijini Tanga na maeneo ya jirani wamekaribishwa kushiriki katika kilele cha maadhimisho kitakachofanyika katika Ukumbi wa Mkurugenzi wa Jiji, ambapo kutakuwa na maonesho, utoaji elimu kwa umma pamoja na fursa ya kujifunza taratibu za kulinda haki zao kama watumiaji.
Jukwaa la Watumiaji Tanzania linaundwa na Mabaraza ya Ushauri ya Watumiaji kutoka mamlaka mbalimbali za udhibiti nchini ikiwemo EWURA CCC, LATRA CCC, TCAA CCC na TCRA CCC, ambayo hushirikiana kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma hizo.




