
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema eneo la Ngorongoro Conservation Area ni urithi wa kipekee wa dunia unaopaswa kulindwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa.
Rais Samia alitoa kauli hiyo leo Machi 12, 2026 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma alipokuwa akipokea ripoti ya Tume iliyoundwa kutathmini matumizi ya ardhi katika eneo la Ngorongoro.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema Ngorongoro imesajiliwa rasmi kama Urithi wa Dunia chini ya UNESCO, hivyo ni wajibu wa Watanzania kuhakikisha wanailinda na kuitunza ili iweze kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Alieleza kuwa eneo hilo lina sifa ya kipekee duniani, ikiwemo uwepo wa bonde kubwa la kreta lenye kina cha takribani mita 600 pamoja na utajiri mkubwa wa bioanuai unaojumuisha aina nyingi za wanyama na ndege.
Rais Samia aliongeza kuwa hifadhi hiyo ni makazi ya wanyama mbalimbali wakiwemo wanaokula majani na wanaokula wenzao, pamoja na ndege wa kuvutia kama flamingo, jambo linalolifanya eneo hilo kuwa moja ya vivutio muhimu vya utalii duniani.

Aidha, Rais Samia alisisitiza kuwa Ngorongoro si tu eneo la utalii bali pia ni sehemu muhimu ya historia ya mwanadamu wa kale. Alitaja maeneo ya Olduvai Gorge na Laetoli ambako wanasayansi wamegundua mabaki na alama za uwepo wa binadamu wa kale zinazokadiriwa kuwa na umri wa takribani miaka milioni tatu.
Kwa mujibu wa Rais Samia, umuhimu huo wa kihistoria na kimazingira unaifanya Ngorongoro kuwa urithi wa thamani kubwa unaopaswa kulindwa kwa uangalifu mkubwa ili kuendelea kuwa kivutio cha kimataifa na hazina ya taifa.

The post Rais Samia Apokea Ripoti ya Matumizi ya Ardhi Ngorongoro Chamwino – Video appeared first on Global Publishers.





