Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ushindani(FCC)William Erio amesema moja ya jukumu la tume hiyo ni kudhibiti bidhaa bandia na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa ya kuvuta wawekezaji hivyo kuwepo na mazingira salama ya biashara yenye ushindani wa haki ni muhimu.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam wakati wa Kikao kazi, Erio pamoja na kutaja shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume hiyo amezungumzia namna wanavyodhibiti bidhaa bandia nchini .
“Sote ni mashahidi Serikali inavyofanya jitihada kuvutia wawekezaji.Mnamsikia Rais kila anapokwenda anavutia wawekezaji,anaongozana na wafanyabiashara, basi haya yote yanaweza kufanikiwa kama bidhaa bandia hakuna na hivyo kutoathiri bidhaa halali ambazo ziko katika mzunguko wa kibiashara.
“Sasa naomba niombe hapa katika kudhibiti bidhaa bandia mojawapo ya kitu kikubwa tunachoomba ni kupata taarifa wapi na nani anashughulika na bidhaa bandia kwasababu wale wanaofanya wanajua biashara wanayofanya sio halali kwahiyo wanazifanya kwa utaratibu wa kificho na hawapiti katika michakato sahihi.
“Ninyi Wahariri mnafanya kazi kubwa na tunaona katika vyombo vya habari mtu amekamatwa na bidhaa bandia hivyo sasa tunaomba mnapopata taarifa mkiwa mnazipeleka katika vyombo vya habari mtujulishe na sisi kwani mkishatoa katika vyombo vya habari hata tunapoenda tunakuta tayari ushahidi umeondolewa,”amesema Erio.
Akielezea zaidi FCC Erio amesema ni taasisi ya Serikali ambayo inashughulika na mambo makuu matatu na ya kwanza ni kuhakikisha wanalinda na kushajihisha ushindani kuhakikisha biashara zinashamiri , uwekezaji unashamiri kama Serikali inavyofanya juhudi katika uwekezaji.
“Hivyo wawekezaji wanakuja wanakuta tayari kuna ushindani uliosahihi ili washindane na kupata faida waliokuwa wameukusudia.Pamoja na hilo tunajukumu la kumlinda mlaji kwa kuhakikisha hapambani na mbinu zozote kandamizi na dhaifu zinazoweza kufanywa na wafanyabiashara katika utendaji wa kazi zao.
“Kwasababu sote tunafahamu dhumuni kubwa la mwekezaji au mfanyabiashara kupata faida,sasa faida unaweza kuipata kwa njia halali au zisizo halali,faida kwa utaratibu unaozingatia sheria au isiyozingatia Sheria
Kwahiyo kazi yetu sisi FCC ni kuhakikisha hayo hayatokei,ushindani unakuwa mzuri lakini,”amesema.
Pia amesema walaji wanalindwa dhidi ya uwepo wa bidhaa bandia kwani ukiwa na wawekezaji anakuwa kwanza amekuja amefanya utafiti wa soko ,amegundua anaweza kuja kufanyabiashara Tanzania ambayo ni nchi salama kwa uwekezaji.
“Basi sisi tunahakikisha akija hayo matarajio yake yanatimia kwa maana hafanyiwi figusu, vurugu na wenzake walioko katika biashara,siku zote tumekuwa tukiueleza umma kwamba Tanzania ni sehemu nzuri ya uwekezaji ,jeografia yetu ni nzuri kwasababu tunapakana na nchi kadha ambapo tunaweza kufanya nao biashara.
“Idadi ya watu wetu ni kubwa kutokana na uwepo wetu katika SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwahiyo kuna soko kubwa la kufanyabiashara na malighafi ambazo zinahitajika zipo na miundombinu ya kutekeleza hayo yote yapo.
“Wote mnaona kwa jinsi gani SGR imebadilisha hali ya uchumi na sasa hivi hata mizigo itakuwa inapita huko ,na naambiwa hadi Desemba SGR itakuwa imefika Tabora kwahiyo wawekezaji wakija wanakuta njia za kuisafirisha bidhaa zao zitakuwepo…
“Lakini na wingi wa Watanzania ambao wanaweza kuwatumia katika viwanda vyao, hivyo uwepo wa FCC unalenga kuhakikisha biashara zao zinakuwa na tija walizokusudia.”