Mkurugenzi wa Gesi Asilia wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mha. Poline Msuya, amesema EWURA inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuhamasisha uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa biashara ya gesi asilia iliyogandamizwa (CNG) ikiwa ni hatua muhimu katika kusaidia juhudi za Serikali za kuchochea matumizi ya nishati safi nchini.
Mha.Msuya ameyasema hayo wakati wa majadiliano ya jopo katika mkutano wa awali wa Mkutano wa 11 wa Mafuta na Gesi wa Afrika Mashariki (EAPCE’25) uliofanyika leo tarehe 04.03.2025 jijini Dar es Salaam. Mkutano husika ambao ni wa siku tatu utaanza rasmi kesho tarehe 05.03.2025.
Ameeleza kuwa moja ya hatua muhimu zilizokwisha kuchukuliwa kuhamasisha uwekezaji ni pamoja na kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye miundombinu muhimu ya CNG, ikiwa ni pamoja na mashine za kushindilia gesi (compressors), vitengo vya kupima gesi (metering units), na hifadhi za CNG (storage cascades) jambo linalovutia uwekezaji zaidi katika sekta husika.