Na Jane Edward, Arusha
Waziri wa wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum Dkt. Doroth Gwajima amesema maandalizi kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yamekamilika kwa asilimia miamoja na wanawake wa Arusha wako tayari kujitokeza kwa wingi kumlaki Mh. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya sheikh amri Abeid jijini Arusha amesema kama wizara inajivunia kazi kubwa iliyofanywa na mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo
Amesema tayari taarifa zimeshawafikia wakaazi wa mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla na ameendelea kusisitiza wanawake kuhudhuria katika siku hii adhimu kwani maadhimisho ya mwaka huu hayatamuacha mwanamke vile alivyokua kwa kumpatia suluhu ya changamoto wanazokabiliana nazo hasa za kujikwamua kiuchumi.
“Kamati zaidi ya tisa zimekaa tangu ilipotangazwa Arusha kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya ili kuhakikisha maadhimisho yanakua ya aina yake na kuleta utofauti wa maadhimisho yaliyopita na haya ya 2025”
Kwa upande wake mhandisi Gladness kitali mratibu wa kitengo cha ushirikishwaji wa wanawake kutoka wizara ya ujenzi amesema katika kusherehekea siku hii wizara ya ujenzi imekuja na mpango wa kuwahamasisha wanawake kushiriki katika shughuli za ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwa ni mpango endelevu.
Amesema kuwa majukumu ya wizara ya ujenzi ni kuhamasisha wanawake katika kazi za ujenzi wa barabara. Kitengo hiki kimeweka mpango mkakati wa kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake ili waweze kushiriki katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara ambapo serikali kupitia sheria ya ununuzi wa umma imeelekeza taasisi zitenge asilimia 30 za manunuzi ya umma kwa ajili ya makundi maalum ambao ni wanawake ikiwemo walemavu
Hata hivyo amesema wizara ya ujenzi inatoa hamasa kwa wanafunzi wa kike kwenye masomo ya sayansi na hisabati kuwa wahandisi au wakandarasi ili waweze kunufaika na sekta ya ujenzi
Amesema hadi sasa wizara ya ujenzi imetembelea wanafunzi zaidi ya elfu tano na kuwatoa hofu wanafunzi wa kike kuacha woga kwani fursa za ujenzi haziangalii jinsia
Siku ya wanawake duniani kwa mwaka 2025 kitaifa inaadhimishwa katika mkoa wa Arusha ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.