Kampuni ya Karagwe Marketing ya Wilayani ya Mkoani Kagera inayojihusisha na Ukoboaji wa zao la Kahawa, imeendelea na kurejesha Tabasamu kwa mabinti wa Shule tofauti za Mkoani Kagera, kwa kuwapatia Taulo za Kike (pedi) ili ziwasaidie kujistiri wawapo katika kipindi cha hedhi, ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upande wa Elimu yenye lengo la kumuinua Mtoto wa Kike kielimu.
Taulo zaidi ya pakiti 300 zimetolewa na Ndg. Devotha Daniel Mkurugenzi wa Kampuni ya Karagwe Marketing Machi 08, 2025 wakati wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wakati alipotembelea Shule ya Sekondari Ruhunga ya Wilayani Bukoba, kwaajili ya kukutana na Wanafunzi hao na kuongea nao, ikiwa ni muendelezo wa zoezi hilo lililoanza tangu Tarehe 01 Machi 2025 kwa kutembelea shule tofauti.
Akiongea na Wanafunzi hao, Devotha amewataka Wanafunzi hasa akina Dada kuongeza juhudi katika masomo yao kwa kujituma zaidi, huku wakizingatia nidhamu ili waweze kufanikiwa katika ufaulu wao kwani Elimu ndio ufunguo wa mafanikio, hivyo hawana budi kutumia muda wao mwingi wakiwa shuleni kujifunza na sio mambo mengine.
“…Mnatakiwa kusoma kwa juhudi ili kufikia malengo yenu, tayari tunaona Rais wetu Dkt. Samia anaweka mazingira wezeshi kwa kutujengea Shule nzuri, kutuletea Walimu, na elimu ni bila malipo hivyo kazi yenu ni kusoma na kufaulu…” amesema Devotha
Licha ya zawadi hizo za Taulo pia Devotha Daniel amekabidhi Mipira minne ikiwemo ya Mpira wa miguu kwa Wavulana, na mpira wa Pete kwa Wasichana ili waweze kuimarisha afya zao kwa kushiriki Michezo Shuleni. Aidha Devotha ametatua moja ya changamoto ya ukosefu wa mashine ya kurudufia mitihani maarufu (photocopy machine) ambapo amekabidhi shilingi Milioni Moja Taslimu kwaajili ya kununulia mashine hiyo.
Wakitoa Shukrani kwa nyakati tofauti baadhi ya Wanafunzi kwa Niaba ya wenzao, wamesema tangu Shule hiyo iwepo yenye zaidi ya Wasichana 329 hakuna Kiongozi wala mgeni aliyewahi kuwakumbuka na kuwaletea zawadi kama hizo, na kuongeza kuwa hali ya hedhi imekuwa ikiwapa shida sana na wakati mwingine kuwaondolea utu wao kutokana na kutokuwa na Taulo za kujistiri
Huu ni Mwendelezo wa Kurejesha tabasamu kwa mabinti kwa mabinti kwa kuzifikia shule kadhaa kupitia kampuni ya Karagwe Marketing ambapo tayari Shule Tatu za Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba zimefikiwa.