NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
MELI ya MV Victoria inayomilikiwa na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO),imepandishwa kwenye chelezo (dry dock) kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kubaini changamoto za kiufundi, hasa katika mitambo,sehemu ya juu ya meli na mwili wa chini wa meli ndani ya maji.
Msimamizi wa Usalama wa Meli na Uhifadhi wa Mazingira,Capt.Bembele Ng’wita,amesema leo jijini Mwanza, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ukaguzi wa meli hiyo.
Amesema hatua hiyo ya ukaguzi huo ni muhimu kwa ajili ya kufanya matengenezo na huduma ya kawaida ili kuhakikisha usalama na ubora wa chombo hicho unaokidhi viwango na sheria za kimataifa.
Capt.Ng’wita amesema “Kufanya ukaguzi wa kina katika maeneo haya kunahakikisha kuwa meli inafanya kazi vizuri na haina matatizo yanayoweza kusababisha ajali au matatizo ya kiusalama kutokana na baadhi ya vifaa kuchakaa.
“Huu ni mchakato wa kawaida katika uendeshaji meli (vyombo vya majini) baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu ili kuhakikisha ufanisi na usalama wa safari zinazofanywa na meli hii.Baadhi ya vifaa vinachoka na vinahitaji huduma na ku-legulaty chombo kirudi katika hali ya kawaida,”amesema.
Capt.Ng’wita amesema ukaguzi unafanyika katika mitambo, pampu,kangavuke (generator), mifumo ya meli kwa maelekezo ya kiwanda kilichoijenga,vitafungwa vipuri ambavyo tayari vimeagizwa na vimewasili.
Kwa mujibu wa Msimamizi huyo wa Usalama wa Meli na Uhifadhi wa Mazingira,baada ya meli kupandishwa juu ya chelezo ukaguzi wa kubaini changamoto za mwili wa meli chini ya maji utafanyika kwa siku tatu.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano kwa Umma wa TASHICO,Anselem Namala,amesema meli ya MV Victoria ilisitisha kutoa huduma Machi 4,mwaka huu,kupisha matengenezo ya kawaida baada ya kutoa huduma kwa mwaka,ilifanyiwa ukaguzi wa ndani na juu, kabla ya kupandishwa kwenye Chelezo Machi 11,2025.
“MV Victoria Hapa Kazi Tu, kupandishwa kwenye Chelezo kunalenga kufanya ukaguzi wa mwili wa meli inapoelea ili kuangalia maeneo yenye changamoto na kuyarekebisha kabla ya kurejea kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria,”amesema.
Namala ameeleza tangu meli hiyo kipenzi cha wananchi wa Kanda ya Ziwa kufanyiwa ukarabati mkubwa,mazingira yalisababisha ikaguliwe,hivyo ili wateja wasipate adaha ya usafiri, mafundi wakishakutatua changamoto zitakazoonekana,chombo kitarudi kutoa huduma ndani ya muda mfupi ujao.
Amesema ukaguzi na maboresho hayo,ni hatua muhimu kwa kuzingatia sheria za kimataifa kuhusu usalama wa meli na kuiweka katika hali nzuri kwa ajili ya safari ndefu.
Meli ya MV Victoria Hapa Kazi Tu ikiwa kenye Chelezo kwa ajili
ya ukaguzi.Meli hiyo iliyofanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 2019,imepandishwa leo
katika Chelezo, Bandari ya Mwanza Kusini.
Msimamizi wa Usalama wa Meli
na Uhifadhi wa Mazingira wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Captain Bembele
Ng’wita,leo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani),kuhusu ukaguzi
wa meli ya MV Victoria baada ya kupandishwa kwenye Chelezo, Bandari ya Mwanza
Kusini, jana.
Kapteni Bembele Ng’wita,Msimamizi wa Usalaama wa Meli na Uhifadhi wa
Mazingira wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO),akizungumza na waandishi wa
habari,kuhusu ukaguzi wa meli ya MV Victoria baada ya kupandishwa kwenye
Chelezo, Bandari ya Mwanza Kusini,leo.
Mkuu wa
Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa TASHICO, Anselem Namala,akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani),leo,baada ya meli ya MV kusitisha huduma
na kupandishwa katika Chelezo kwa ajili ya ukaguzi.Picha zote na Baltazar
Mashaka