Na John Walter -Babati
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, ameonya vikali matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akisema yanaweza kusababisha chuki na mvurugano, jambo ambalo linaweza kuleta taswira mbaya kwa chama.
Akizungumza leo Machi 12, 2025, ofisini kwake mjini Babati, Mheshimiwa Toima amesisitiza kuwa chama kina utaratibu wake wa kuwasiliana na umma, ambapo ni viongozi wa ngazi mbalimbali walioidhinishwa pekee ndio wanapaswa kuzungumza kwa niaba ya chama.
Ameeleza kuwa maamuzi yote ya chama hutokana na vikao rasmi vinavyotambulika kisheria, na si kila mwanachama au mpenzi wa chama anaruhusiwa kutoa matamko kiholela mitandaoni.
Ametoa onyo kali kwa wale wenye tabia hiyo, akiwataka waache mara moja.
Aidha, amesisitiza kuwa wabunge na madiwani waliopo madarakani bado wanatambulika na chama hadi muda wao wa uongozi utakapomalizika rasmi, hivyo hakuna haja ya kuwakashifu au kuwachafua mitandaoni.
“Hatupendi kusikia mtu anamkashifu kiongozi wa chama kwenye mitandao ya kijamii kwa namna yoyote ile, tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu, ni muhimu kuheshimu taratibu za chama na kuepuka kulichafua kupitia malumbano yasiyo na tija,” amesema.
Mheshimiwa Toima ametoa wito kwa wanachama wa CCM kuhakikisha wanadumisha mshikamano na nidhamu ndani ya chama, na kwamba kama mtu ana tofauti na mwingine, asitumie jina la chama kufanikisha malengo binafsi au kuchafua taswira ya chama.