Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Songwe
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kupitia Makamu Mwenyekiti wake Tanzania Bara Stephen Wasira amesema Chama hicho hakitakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote anayetaka kuvuruga Umoja na amani iliyopo nchini.
Wasira alitoa kauli hiyo leo Machi 14,2025 alipokuwa akizungumza na wana CCM pamoja na wananchi wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu yenye lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kuzungumza na wana CCM.
“Msingi wa CCM ni umoja na mshikamano na hata vyama vya TANU na Afro Shiraz Part (ASP) vilipoamua kuanzisha Chama hiki pamoja na mambo mengine waliweka msingi wa kuwa wamoja.
“Sisi ni Chama Cha Mapinduzi, sijui hawaelewi? CCM ni muunganiko wa vyama viwili. Ni vyama ambavyo vimetuletea msingi wa umoja na tulileta uhuru na umoja. Hata maneno yaliyopo katika nembo ni Uhuru na Umoja…
“Hivyo tunataka nchi yetu iendelee kuwa huru lakini wawe wamoja na katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wetu tumesimamia amani ya nchi yetu. Ndio maana sisi ni tofauti na nchi nyingine ambazo zimepigana na nyingine bado zinaendelea kupigana,” amesema.
Ameongeza ukiona vinaelea ujue vimeundwa na umoja na amani iliyopo nchini imeundwa na TANU pamoja na Afro Shiraz Party, lakini pamoja na waasisi wa taifa hili na kuongeza hata maendeleo yaliyopo nchini yametokana na umoja uliopo.
Amesisitiza kwamba wanaweza kuvumilia yote lakini kwa mtu anayetaka kuvunja umoja hawatamvumilia, anayetaka kuvunja amani ya nchi hawatamvumilia na kwamba wanaotawala ni CCM lakini wanawaambia hawatavumilia kuona Umoja uliopo unaharibiwa.
“CCM hatuna Polisi lakini tunayo serikali na haitakuwa tayari kuona amani, umoja na mshikamano wetu unatoweka kwa namna yoyote.Tunayasema haya kwa sababu tunajua wapo watu ambao wapo nje ya Tanzania na wengine ni wajukuu wa waliotutawala wanataka kuharibu amani ya nchi yetu.Hatuwezi kukubali.”
Kuhusu wanaosema CCM imekaa sana madarakani amewakumbusha kuwa hakuna mahali ambapo walikubaliana nao kwamba CCM itakaa kwa muda gani na kwamba kazi ya kuleta maendeleo ya wananchi haina ukomo, hivyo wataendelea kuwepo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.
“Nataka tuelewane, wanaosema tunakaa sana watujibu tulipatana tutakaa kwa muda gani. Tulidai uhuru ili kubadilisha maisha ya watu, na maisha hayana mwisho anakufa mmoja na maisha yanaendelea, hiyo ndio kazi yetu
“Tulipotangaza maadui watatu ujinga, umasikini na maradhi maana yake tulitangaza vita ya kudumu. Kwa hiyo nadhani wasituulize ilimradi Watanzania wanatuamini tutaendelea kuwepo, ma hakuna dalili za sisi kutoaminika, kwa hiyo tunawambia mambo tunayofanya sasa hivi lengo lake ni maendeleo ya watu,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira akizungumza na wana CCM katika ukumbi wa Kanisani Vwawa Wilaya Mbozi mkoani Songwe akiwa kaika ziara ya kikazi kukagua uhai wa Chama na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
VIONGOZI na wanachama wa CCM Mkoa wa Songwe wakicheza na kushangilia walipokuwa wakimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira katika Ukumbi wa Kanisani, Vwawa wilayani Mbozi Mkoa Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo akiwasilisha tarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa ndani ikiwa sehemu ya ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira katika Ukumbi wa Kanisani Vwawa, Wilaya Mbozi mkoani Songwe.