Na Mwandishi Wetu, Songwe
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Stephen Wasira amesema kwa mfumo wa sasa wa Chama hicho kupata wagombea wake wa uchaguzi mkuu mgombea yeyote atakayehonga ilia pate nafasi ajue atafilisika na atakufa kwa presha.
Akizungumza na wana CCM wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ,Wasira amesema Chama hicho pamoja na mambo mengine kimekuwa na utaratibu wa kujisahihisha na ndio maana wamebadilisha mfumo wa upigaji kura kupata wagombea ndani ya chama kwa kuongeza idadi ya wapiga kura.
“CCM imeongeza wigo wa demokrasia kwa kuwa na idadi kubwa ya wajumbe wa kupiga kura, ukihonga basi utahonga hadi utafilisika,utaugua na utakufa kwa presha.Ndio maana tunawaambia chama chetu waje wagombea watatu kisha tuchague mmoja halafu tuende kwa wanachama.
Amefafanua awali wajumbe waliokuwa wanapiga kura walikuwa wachache na baadhi ya maeneo walikuwa wapiga kura 600 hadi 800 lakini kwa mfumo wa sasa baada ya kufanyika mabadiliko wajumbe wameongezwa , hivyo wako wengi na hata akitokea Mgombea akataka kuhonga ajue atafilisika na hatapata.
Ametoa mfano kuna majimbo wajumbe ambao wanapiga kura ya kuchagua wagombea ndani ya Chama wanafika mpaka wajumbe 17000 , hivyo atakayeamua kuhonga wajumbe ili apate nafasi ajue atahonga mpaka atafirisika, ataugua na atafariki kwa presha.
“Kuna wakati nilienda Zanzibar vijana wakaniambia wanataka kugombea ubunge nikawaambia ubunge unanunuliwa kwa fedha nyingi.Vijana mnasema mnaakili lakini hawa watu wanataka fedha.
“Hivyo nikawaambia vijana tunataka kuweka mfumo ambao utawezesha vijana Kwenda bungeni bila kuhonga fedha.Tukiacha mfumo ambao mtu akitoka machimbo anauliza wako wajumbe wangapi?Amehoji Wasira na kuongeza haiwezekani kuwa na CCM ya kununua ongozi kwa Sh.100,000.”
Wasira amesema CCM inataka kuwa na viongozi wanaosimamia maslahi ya wananchi ili kuendelea kuwa chama kinachoheshimika duniani.
Pia imefika wakati mgombea akikosa nafasi ya kuteuliwa anasema ana watu wake na kuendeleza makundi.“Sasa unasema una watu wako mo wawapi.Hakuna mwenye watu wake.
“Katika watu watatu akipatikana mmoja wengine mnaungana na aliyechaguliwa, hivyo tunawaomba wanachama wetu nchi nzima tuache makundi, ukigombea ukishindwa ukubali na kama hutaki kushindwa usigombee.”
Amesisitiza lazima CCM na viongozi wake wawe imara, kusiwe na makundi na kuongeza Chama hicho ni daraja kati ya wananchi na Serikali, hivyo wataendelea kusikiliza kero na changamoto ili zipatiwe ufumbuzi.