Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, Mboni Mhita (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Meneja Msaidizi huduma mkoa wa kikodi wa Kahama, George Kazumba kama ishara ya ushirikiano wao katika kazi wakati wa ziara ya maafisa kutoka TRA Wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na Maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA (hawapo pichani), wakati maofisa hao walipofika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha wakati wa zoezi la kutoa elimu ya kodi ya Mlango kwa Mlango kwa wafanyabiashara
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, Mboni Mhita (mwenye koti jekundu) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa mbali mbali kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa ziara ya maafisa kutoka TRA Wilayani humo.
MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mboni Mhita amewataka wananchi kuendelea kulipo kodi na kujivunia maendeleo mbalimbali yanayopatikana kutoka na kodi wanazolipa.
Mboni ameyasema hayo leo Machi 18, 2025 alipokutana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliofika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha wakati wa zoezi la elimu ya kodi ya mlango kwa mlango inayoendelea wilayani hapo.
Amesema ndani ya Wilaya kuna miradi mbalimbali ambayo inatokana na kodi wanazolipa
“Kodi ambazo tunalipa ndio ambazo zinatumika na serikali kwenda kufanya maandaleo haya katika jamii… sisi wa Kahama tunajivunia hospitali ya kisasa ambayo utazani ni ya kanda, ukiangalia zahanati za kisasa katika wilaya yetu”
Kwa upande wake Ofisa mkuu Msimamizi wa kodi kutoka TRA ambae ni kiongozi wa timu hiyo Lameck Ndinda ameeleza kuwa lengo la zoezi hilo ni kutoa elimu ya kodi na kusikiliza changamoto na maoni ya wafanyabiashara ili kuweza kuboresha huduma zao
Aidha Ndinda amefafanua kuwa katika zoezi hilo wamebaini kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara bado hawajakadiriwa na na wengine kutokutoa risiti vizuri hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara kwenda kukadiriwa kabla ya tarehe 31 Machi ili kuepuka adhabu.
” Wito wangu kwa wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kwenda kukadiriwa kabla ya tarehe 31 mwezi Machi, na wakisha kukadiriwa wawahi kufanya malipo ya awamu ya kwanza.”
Nae, mmoja wa wafanyabiashara hao Tumaini Kinanda amesema zoezi hilo linasaidia kuboresha mahusiano kati ya TRA na wafanyabiashara na ameomba zoezi hilo liwe endelevu ili waweze kujifunza zaidi mambo mbambali ya kodi.