.jpeg)
Dar es Salaam, Tanzania – Machi 18, 2025 – Wingu Group Tanzania imefanikiwa kuzindua awamu ya pili ya upanuzi wa kituo chake cha ‘data’, hatua muhimu inayothibitisha dhamira yake ya kuimarisha miundombinu ya kidijiti na kuendeleza mabadiliko ya kidijitali nchini.
Awamu hii mpya inajengwa juu ya mafanikio ya awamu ya kwanza iliyokamilika mwaka 2022. Kwa kuwa kituo cha data hiki ni cha upande wowote, wateja sasa wanaweza kufurahia upatikanaji wa chaguzi mbalimbali za muunganisho wa mtandao bila kizuizi kutoka kwa mtoa huduma mmoja. Kujumuishwa kwa vyumba viwili vya mkutano wa waendeshaji (Meet-Me Rooms) kunarahisisha muunganisho wa watoa huduma mbalimbali wa mtandao, kuongeza ufanisi na kuboresha uzoefu wa watumiaji.
Usalama na uhakika wa ufanisi wa kituo hiki pia umeboreshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya usalama wa kimwili na wa kidijitali. Mfumo wa usambazaji wa umeme wa UPS wa hali ya juu unahakikisha kuwa shughuli haziingiliwi, huku makubaliano ya kiwango cha huduma (SLA) yakihakikisha uthabiti wa miundombinu.
Akizungumza kuhusu mradi huu wa upanuzi, Anthony Voscarides, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Wingu Group Tanzania, alisema: “Kituo chetu cha data cha upande wowote kinaakisi dhamira yetu ya ubora na uvumbuzi. Kimeundwa kwa ajili ya kushughulikia mahitaji yanayoongezeka ya shughuli za kisasa za kidijitali na kitasukuma mbele maendeleo ya teknolojia katika eneo letu.”
Tangu kuanzishwa kwake, Wingu Group Tanzania kimejidhihirisha kama kiongozi katika sekta ya vituo vya’ data’ vya kisasa, na upanuzi huu unasisitiza uwekezaji wake wa kimkakati katika miundombinu ya hali ya juu. Hatua hii haitainua tu viwango vya huduma kwa wateja, bali pia itachochea ubunifu wa baadaye kwa manufaa ya sekta mbalimbali.
Upanuzi huu unaashiria hatua mpya katika safari ya Wingu Group nchini Tanzania, kikithibitisha nafasi yake kama kinara wa miundombinu ya kidijitali na mdau muhimu katika maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kidijitali nchini.