Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira ameitaka serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuangalia uwezekano wa ardhi inayomilikiwa na mwekezaji Mohammed Enterprises Ltd wilayani Rungwe mkoani Mbeya kama imemshinda na haizalishi irejeshwe serikalini ipangiwe matumizi mengine.
Wasira alitoa kauli hiyo baada ya wananchi wa Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya kudai kuwa Mohammed Enterprises Tanzania Ltd, anamiliki eneo kubwa la mashamba ya chai lakini kwa muda mrefu hajalipwa na hivyo kuwa mapori makubwa yanayoishi nyoka na wanyama waharibifu wakati wananchi hawana maeneo ya kulima.
Hivyo kutokana na kutelekezwa kwa mashamba hayo na kuwa mapori wanaiomba CCM kuielekeza serikali imnyang’anye ili wapate maeneo ya shughuli za kilimo.
Akizungumza wakati akisalimia wananchi wa eneo hilo akiwa katika mwendelezo wa ziara yake mkoaNI huMo, Wasira alisema Chama kinaiambia serikali kupitia kwa Waziri wa Kilimo kuwa, aridhi hiyo kama Mohammed Enteprises imemshinda airudishe serikalini halafu serikali itajua namna ya kufanya.
Alisema kwa sababu sheria ya umilikaji wa ardhi inaeleza wazi kuwa ukipewa ardhi ni lazima uzalishe kukuza uchumi kwa kuwa kama mashamba hayo hayazalishi maana yake hata viwanda vya chai navyo haviwezi kuzalisha na matokeo yake uchumi wa wananchi unadidimia.
“CCM hatufanyi kazi ya kudidimza uchumi bali tunao wajibu wa kuhakikisha uchumi wa wananchi unakuwa. Serikali ina sheria inayozungumzia umiliki wa ardhi, kama ni mkulima mkubwa umepewa ardhi ulime maana yake kuna watu wengine hawatakuwa na ardhi hiyo kwa maana umepewa ulime sasa masharti ya kumiliki lazima utekeleze yale uliyokubali. Kama wewe ni mkulima wa chai na umepewa mashamba ya chai ili ukuze uchumi lazima ulime chai, uitunze na uzalishe.
“Ukiacha kufanya hivyo unavunja mkataba, hakuna mtu anayeruhusiwa kumiliki ardhi, ndiyo maana katika historia yetu tulikataa sheria ya Kingenereza iliyokuwa inaitwa ‘Free Hold’ ambayo ilikuwa inampa mmiliki haki ya kumiliki ardhi hata kama hafanyi chochote na anamiliki milele.
“Hakuna mtu mwenye uwezo kumuondoa lakini sheria hiyo ilifutwa mwaka 1962 ndipo tukaanzisha sheria ya ‘Lease hold’ kwamba wewe ukipewa ardhi haiwi yako, na masharti ya kukodi lazima uwe unafanya kile ambacho umeaihidi kukifanya.
“Sasa kuna Mohamed Enteprises ana ardhi, ana mashamba ya chai hapa Rungwe lakini yameachwa yamekuwa pori. Tunataka kuiambia serikali kutokea Rungwe na kupitia kwa Waziri wa Kilimo, ardhi hii kama Mohammed Enteprises imemshinda na haizalishi airudishe serikalini ili ipangiwe matumizi mengine kwa jinsi itakavyoona inafaa,” alisema.
Aliongeza kwa sababu sheria ya umilikaji wa ardhi ukipewa lazima uzalishe na kimsingi hakuna mgogoro na Mohamed Enterprises ila wana mgogoro wa utekelezaji wa sheria ya uzalishaji, utekekelezaji wa sheria wa kutumia aridhi iliyokodishwa.
Wasira alisema ardhi ya Tanzania ni mali ya wote na Rais amepewa mamlaka ya kuisimamia kwa niaba ya Watanzania, ndio maana kwa anayeshindwa kuiendeleza Rais anayo mamlaka ya kuitwaa.
“Sasa sisi tunamwambia Waziri wa Kilimo maana siwezi kumwagiza Rais, mimi naiagiza serikali kwa maana ya Wizara ya Kilimo ichukue hatua ya kumaliza jambo hili haraka ili tuitumie ardhi ile na itumike kwanza katika mazingira ya Rungwe ambako ardhi ni ndogo.
“Ukiwa nayo wewe ardhi kubwa halafu haitumiki inakuwa dhambi maana watu wengine hawana kwa sababu wewe unayo halafu na wewe huitumii, hiyo sio sawa. Kwa hiyo tunakwenda kufuatilia na kwa kweli nitazungumza na Waziri wa Kilimo kuhusu jambo hili.”