Na Mwandishi Wetu, SONGWE
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa 614 Local Miners Songwe wamempa tuzo Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Solomon Itunda ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuimarisha mahusiano ndani ya Wilaya hiyo pamoja na kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo.
Wachimbaji hao wamemkabidhi Mhe. Itunda tuzo hiyo Jumanne Machi 18, 2025 katika hafla ya kukabidhi madawati 100 yenye thamani ya Shilingi Milioni 15 yaliyotolewa na wanachama wa 614 Local Miners Songwe kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa Shule ya Msingi Saza.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao, Mwenyekiti wa 614 Local Miners, Dickson Kadinda amesema kuwa tuzo hiyo wameitoa kutokana na namna Mkuu huyo wa Wilaya anavyoimarisha mahusiano kati ya wachimbani na wananchi, viongozi pamoja na kutatua migogoro ya wachimbaji inayotokea katika Wilaya hiyo.
“Sisi wachimbaji wadogo wa 614 Local Miners tumeamua kukupa tuzo hii kutokana na unavyosaidia kuimarisha amani, mahusiano kati ya wachimbaji na jamii, wachimbaji wamepitia changamoto nyingi lakini umekuwa nasi ukionyesha ushirikiano mkubwa. Kwa pamoja tunasema tunakushukuru sana” ameeleza.
Amesema kuwa katika maeneo ya uchimbaji wa madini wilayani humo, migogoro ikiibuka Mkuu wa Wilaya huyo amekuwa mstari wa mbele kuwaita wachimbaji, kuwasikiliza kisha kupata suluhisho hali ambayo imesaidia wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhe. Itunda amesema “Ninawashukuruni sana ndugu zangu (wachimbaji). Nimeipokea tuzo hii kwa moyo wa shukrani. Kikubwa yote tunayoyafanya ni katika kumsaidia Rais wetu Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Yeye ndiye kinara wa kuimarisha mahusiano hivyo hata sisi wasaidizi wake tunafanya kuendana na kile alichotutuma hasa kuhakikisha tunashikamana na kuwa wamoja” amesema DC Itunda na kuongeza;
“Binafsi ninaamini kuwa changamoto zinazojitokeza tutaendelea kuzitatua kwa njia ya kukaa pamoja na kuzungumza. Utulivu mnaouona unatokana na namna Rais wetu anavyoendelea kuimarisha mahusiano kati ya makundi mbalimbali. Ninawaomba tumuunge mkono Rais wetu”.
Mhe. Itunda amempongeza Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mahusiano hususan kupitia falsafa yake ya 4R.