-Alivyoleta tabasamu uwezeshaji mikopo elimu ya juu
Na: Dk. Reubeni Lumbagala
Leo, Machi 19, 2025, imetimia rasmi miaka minne tangu Dk. Samia Suluhu Hassan alipoapishwa Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Pombe Magufuli.
Rais Dk. Samia amekuwa na kazi ya kuendelea kazi zilizoanzishwa na mtangulizi wake lakini pia kuja na mikakati yake ili kuendeleza gurudumu la maendeleo ambalo ndiyo wajibu wa serikali kwa wananchi wake.
Sekta ya elimu imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ili kuhakikisha wanafunzi wa Kitanzania wanapata elimu bora itakayowawezesha kuendeleza maisha yao hasa baada ya kuhitimisha masomo yao.
Katika kuangazia mafanikio ya elimu nchini, makala hii imejikita kuona uwezeshaji uliofanywa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu ili kuhakikisha wanafunzi hao wanasoma katika mazingira mazuri.
KUONGEZEKA KWA FEDHA YA KUJIKIMU
Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuongeza fedha ya kujikimu kwa siku kutoka shilingi 8,500 hadi 10,000. Kutokana na kuongezeka kwa gharama za maisha, serikali ilisikia kilio cha wanafunzi wa vyuo walioomba fedha ya kujikimu iongezeke kwani fedha hii ndiyo inayowasaidia kupata chakula na kulipia gharama za malazi. Kazi nzuri hii imefanyika chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
WANAFUNZI WA STASHAHADA KUPATA MIKOPO
Ilikuwa ni kilio na ombi kwa wanafunzi wa ngazi ya Stashahada (Diploma) kunufaika na mikopo kama ilivyo kwa wanafunzi wa ngazi ya Shahada (Degree). Kwa kuanzia, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, wanafunzi 9,959 wa ngazi ya Stashahada wamenufaika na mikopo. Serikali inaendelea na mikakati ya kuongeza fedha zaidi ili kuongeza idadi kubwa zaidi ya wanufaika wa mikopo kwa ngazi Stashahada. Ni katika uongozi huu wa Serikali ya Awamu ya Sita, ndipo wanafunzi wa ngazi ya Stashahada walipoanza kunufaika na mikopo.
SAMIA SCHOLARSHIP YALETA KICHEKO
Katika kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu hasa kwa wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi na ya kipaumbele, serikali ilianzisha ufadhili maalum ujulikanao kwa jina la “Samia Scholarship” ambapo kwa mwaka 2022/2023, wanafunzi 3,696 wamenufaika na mikopo hiyo. Ufadhili huu ni nyenzo ya kutoa hamasa kwa wanafunzi kusoma kwa bidii ili wafaulu kwa viwango vikubwa hatimaye wawe miongoni mwa wanufaika. Pia, ufadhili huu unaongeza idadi ya wataalam nchini katika programu mbalimbali ili kusaidia kufanikiwa kwa mikakati ya maendeleo iliyopo.
KUONGEZEKA BAJETI YA MIKOPO KILA MWAKA
Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa sikivu sana kwani kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya mikopo, na serikali imekuwa ikiendana na uhitaji uliopo kwa kuongeza fedha kila mwaka. Kwa mfano, kwa mwaka 2021/2022, serikali ilitoa shilingi Bilioni 570. Mwaka 2022/2023, serikali ikatoa Bilioni 654, mwaka 2023/2024 Bilioni 749 na mwaka 2024/2025 Bilioni 787. Ni dhahiri kuwa kuongezeka kwa fedha za mikopo kila mwaka ni matokeo ya serikali kuipa kipaumbele sekta ya elimu ambayo ni muhimu katika kufanikisha mipango na mikakati ya kimaendeleo nchini.
KUONGEZEKA KWA IDADI YA WANUFAIKA WA MIKOPO KWA UJUMLA
Ongezeko la fedha za mikopo kumeakisi ongezeko la idadi ya wanafaika wa mikopo kila mwaka. Katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, wanufaika wameongezeka sana. Mathalani, mwaka 2021/2022, walionufaika ni 177,892, mwaka 2022/2023, walionufaika 202,016, mwaka 2023/2024, walionufaika 228,122 na mwaka 2024/2025, wanufaika wamefikia 245,799.
WANAFUNZI WANUFAIKA WA MWAKA WA KWANZA WAMEONGEZEKA SANA
Katika miaka hii minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, wanufaika wa mikopo wapya yaani wa mwaka wa kwanza wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka. Mathalani, mwaka 2021/2022, wanafunzi 70,609, mwaka 2022/2023, wanafunzi 72,979. Kwa mwaka 2023/2024, wanafunzi 88,000 na mwaka 2024/2025, wanafunzi 89,627. Ongezeko hili la wanufaika wapya wa mwaka wa kwanza linatokana na kuongezeka kwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi.
KUONGEZEKA MAKUSANYO YA MIKOPO ILIYOIVA
Miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha njia za ukusanyaji wa mikopo iliyoiva hasa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Kwa mfano, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia Machi 2021 hadi Februari, 2025, ongezeko la maikoponikiyoiva imefikia Bilioni 650.25.
Kwahiyo, katika kusherehekea miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita madarakani, uwezeshaji wanafunzi wa elimu ya juu umefanikiwa sana na hivyo kusaidia kutimiza ndoto za vijana wengi kupata elimu ya juu.
Maoni: 0620 800 462