Wananchi wa Jimbo la Mchinga Manispaa ya Lindi wamehimizwa kutunza na kuilinda miundombinu ya maji Iliyojengwa na inayoendelea kujengwa Jimboni humo ili iwe endelevu na kuendelea kutoa huduma.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo hilo na mke wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Salma Rashid Kikwete pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva Katika maadhimisho ya Wiki ya maji Kiwilaya ambapo kwa Wilaya ya Lindi imefanyika katika Jimbo la Mchinga.
Katika maadhimisho hayo Mbunge Salma Kikwete ameweka jiwe la Msingi mradi wa maji uliopo katika kitongoji cha Runyu Kata ya Kitomanga wa uchimbaji wa visima 5 na ujenzi wa viosk vya maji kupitia program ya visima 900 iliyolenga kuhakikisha kuwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi waishio maeneo ya vijijini wanapata huduma ya maji safi na Salama kupitia maono ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Aidha, Mbunge huyo wa Mchinga Salma amewaomba RUWASA kuviingiza kwenye mpango wa kupata maji vijiji ambavyo vimesalia kufikiwa na huduma ya maji kwenye jimbo hilo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa jimbo la Mchinga Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini RUWASA Wilaya ya Lindi Mhandisi Athanas Patrick Lume amesema mradi huo wa visima 5 utanufaisha zaidi ya Wakazi 2,651 katika vijiji vitatu vya Dimba, Makangara na Ruchemi na vitongoji 2 ambavyo ni Runyu na Likonde huku akieleza kuwa mpaka sasa jumla ya visima 4 vimechimbwa na kuanza kupata maji ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na Salama na kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji.
Pia amesema katika kipindi cha miaka minne kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2025 Serikali imeidhinisha jumla ya shilingi Bilioni 5.71 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 17 ikiwemo hiyo miradi 5 ya uchimbaji wa visima na ujenzi wa viosk na kwamba hadi kufikia Februari 2025 wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji safi jimboni humo ni asilimia 77 kutoka chini ya asilimia 30.
Wananchi wa Kitongoji cha Runyu wakiongozwa na Diwani wa kata ya Kitomanga wameeleza namna walivyofurahishwa kwa hatua hiyo ambayo inakwenda kuwapa unafuu na kuwapunguzia mwendo wa kufuata maji ambayo wenyewe wanadai wakitumia pamoja na wanyama.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Uhifadhi wa uoto wa asili kwa uhakika wa maji” ikitafsiriwa kwa vitendo kwa upandaji wa miti kuzunguka mradi huo.