Na: Calvin Gwabara – Mvomero.
Kufuatia taarifa za athari kubwa
za Nzi Weupe kwenye mazao ya mbogambona Wilayani Mvomero zilizoibuliwa na
wakulima wakati wa utekelezaji wa mradi wa AGRISPARK Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru ameahidi
kutuma timu ya wataalamu kwenye wilaya hiyo kuona athari na kufanya oparesheni
ya kuwatokomeza wadudu hao.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru (Picha kwa msaada https://afrikaleo.co.tz/) |
Mkurugenzi huyo mkuu wa TPHPA amesema
amesikia taarifa zilizolipotiwa na vyombo vya habari kuhusu kilio cha wakulima
wa Nyandira, Wilaya ya Mvomero, Mkonai Morogoro lakini hakuna taarifa rasmi
iliyowasilishwa na Halmashauri kwenye ofisi yake kwaajili ya kuhitaji msaada kwenye
kuwakabili wadudu hao ambao wanashambaulia mazao ya wakulima.
“Sisi tunafanya kazi nchi nzima
katika kupambana na majanga ya wadudu mbalimbali na ndege ambao wanaathiri
mazao ya wakulima lakini utaratibu unaotakiwa kufuatwa ni Maafisa ugani wa kata
kupeleka taarifa kwenye ofisi za halmashauri, halafu halmashauri
wakishajiridhisha wanatakiwa kutuandikia barua kuomba msaada wetu na sisi huwa
tunachukua hatua mara moja maana hata hivi sasa wataalamu wetu wapo kwenye
mikoa mbalimbali wakifanya kazi hizo kusaidia wakulima” Alisema Prof. Ndunguru.
Aliongea “Tunamshukuru sana Rais
wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya Kilimo kwa kuendelea
kuiwezesha TPHPA kwa kutupatia zana za kisasa za kupambana na visumbufu vya
mimea kwa kutupatia Madawa ya Ruzuku lakini pia vitendea kazi ikiwemo ndege
zisizo na rubani (Drone) na ndege kubwa kwaajili ya kupulizia dawa kwenye mazao
na hii inatusaidia kuwafikia wakulima
wengi zaidi tofauti na awali”.
Prof. Ndunguru amesema kuwa
taasisi yake ipo kwaajili ya kuwahudumia wakulima pale wanapopatwa na majanga
makubwa ya wadudu na magonjwa ambayo yanahitaji vifaa na uwezo mkubwa wa
kupulizia madawa hivyo wanapopata changamoto hizo wasisite kufuata taratibu ili
waweze kusaidiwa kwa haraka.
Amesema hivi karibuni wanatarajia
kupokea ndege nyingine moja kubwa ya kisasa kwaajili ya kuongeza nguvu katika
kupulizia dawa kwenye mazao kwa kuwa tayari imeshalipiwa na itawasili muda
wowote kuanzia sasa ili kusaidia ndege moja kubwa waliyonayo hivyo wanatarajia
itaongeza sana ufanisi katika kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea.
Kwa upande wake mtafiti Mkuu
mweza wa mradi wa AGRISPARK –SUA Dkt. Nicholous Mwalukasa ambao vilio hivyo wa
wakulima vilitolewa mbele yao na kuomba wawasaidie kupaza sauti zao kwa
serikali amesema taarifa hiyo ya TPHPA wataifikisha kwa wakulima na maafisa
Ugani kwenye kata hizo ili waweze kufuata taratibu zilizoanishwa na kuweze
kusaidiwa.
![]() |
Kwa upande wake mtafiti Mkuu mweza wa mradi wa AGRISPARK –SUA Dkt. Nicholous Mwalukasa akizungumza na wanafunzi wa mradi huo mara baada ya kuzungumza na wakulima kuhusu changamoto hiyo. |
“ Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa
TPHAPA Prof. Ndunguru kwa kuamua kuchukua harua za haraka kuwasaidia wakulima
hao mara tu baada ya kumfikishia taarifa hizo na tunaamini wakulima hao
wataweza kupata suluhisho changamoto hiyo ya wadudu na kulima kilimo chenya
tija” alisema Dr. Mwalukasa.
Aliongeza “Kwa mujibu wa Prof.
Ndunguru amesema zipo njia rahisi zaidi zinazoweza kutumiwa na wakulima katika
kudhibiti wadudu hao hivyo sisi kama mradi tutafuatilia tuzipate na kisha
kuandaa vitabu vidogo ambavyo wakulima watapewa na kuweza kupambana na wadudu
hao”
Wakulima wa mbogamoga Kata ya
Nyandira wilayani Mvomero waliibua na kuwasilisha changamoto hiyo ya wadudu kwa
Watafiti wa mradi wa AGRISPARK waliokuwa kwenye wilaya hiyo kwa lengo la
kuzungumza na wakulima kupata changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kutokana
na machapisho mbalimbali ya kisayansi yaliyopo na watafiti wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo waliobobea kwenye maeno hayo.
Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali ya jamahuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama maono
mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwaajili ya kuwawezesha
watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
![]() |
Muonekano wa Nzi weupe wakiwa kwenye mmea picha kwa hisani ya mtandao. |