Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Songea
JUKWAA la Wahariri Tanzania(TEF) limemchagua Deodatus Balile kuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo huku Bakari Machumu akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
Mwenyekiti Balile kabla ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya kwa miaka minne alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo ambapo kwa mujibu wa kanuni ya Uchaguzi wa TEF kifungu namba 8 na 9 ,ametangazwa kuwa mshindi kwa kuwa mgombea pekee na hakuna aliyekuwa ameweka pingamizi kugombea katika nafasi hiyo.
Kwa upande wa Machumu naye alikuwa mwenyewe akigombea nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa TEF na hivyo amechaguliwa kwa kishindo.
Kabla ya Machumu kutangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti mpya kwa miaka minne ,alikuwa akishika nafasi hiyo ambayo amefanikiwa kurejea katika nafasi hiyo.
Akizungumza leo Machi 5,2025 wakati akitangaza matokeo ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo la Wahariri Tanzania,Mwenyekiti wa Uchaguzi huo uliofanyika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Mjini Songea mkoani Ruvuma, Frank Sanga amelitoa sababu za wagombea hao kupitishwa bila kupigiwa kura .
“Kamati ya Uchaguzi tulikuwa tumejiandaa vizuri na tulikuwa tumetengeneza karatasi za kupigia kura lakini wagombea kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hawakuwa na pingamizi wala wagombea wengine.
“Hivyo kwa kutumia kifungu cha kanuni namba 8 na 9 iwapo mgombea atakuwa mmoja na hana pingamizi basi atatangazwa kuwa mshindi.Hivyo tunamtangaza Deodatus Mutalemwa Balile kuwa Mwenyekiti wa TEF.Pia namtangaza Bakari Steven Machumu kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kutumia kanuni ile ile.”
Wakati Balile akitangazwa kuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo wahariri walilipuka kwa shangwe kuonesha kufurahishwa na ushindi wake na wakati akiomba kura Balile alisisitiza iwapo atashinda atashirikiana na kamati ya utendaji ya jukwaa hilo pamoja na wanachama wa jukwaa hilo kuendelea kujenga misingi ya taaluma ya habari lakini pia kuwa na jukwaa kuwa na uwezo kiuchumi na kuweza kujitegemea
Naye Makamu Mwenyekiti Machumu ameahidi kuutumia muda wake kutoa ushauri utakamuwezesha Mwenyekiti na kamati ya utendaji kuhakikisha jukwaa hilo linatimiza majukumu yake huku akisisitiza kuwa atahakikisha anasimamia mabadiliko ya kiuchumi kwa vyombo vya habari kwa kujikita katika teknolojia ya habari kwa digitali.