NA WILLIUM PAUL, SAME.
JIMBO la Same mashariki lilianzishwa mnamo mwaka 1995 ambapo lilizaliwa na Jimbo la Same hivyo ni moja ya majimbo mawili yanayoiunda wilaya ya Same na ni moja ya majimbo tisa yanayounda mkoa wa Kilimanjaro.
Jimbo hili linaundwa na kata 14 ambapo kata 5 ziko ukanda wa Tambarare na kata 9 ziko ukanda wa milimani aidha lina vijiji 49 vyenye kaya 131350.
Mbunge wa Jimbo hilo ni mwanamama shupavu Anne Kilango Malecela kupitia Chama cha Mapinduzi ambaye amekuwa akipambana usiku na mchana kuhakikisha maendeleo yanapatikana ndani ya Jimbo hilo akisaidiana na Serikali.
Wananchi wa Jimbo hilo kwa kiasi kikubwa wanajishughulisha na shughuli za kilimo cha Mpunga, Tangawizi, Mahindi, Maharagwe, Karanga, Ndizi, Kahawa, matunda na hata miti kwa ajili ya mbao.
Mbunge Anne anadai kuwa, Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 imeweza kutekelezwa kwa vitendo katika Jimbo hilo ambapo katika kipindi cha miaka mitano wamepokea fedha shilingi 105,852,455,280.62 kwa ajili ya kutekelezwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Anadai kuwa, katika sekta ya Elimu, Jimbo hilo limepokea fedha shilingi 7,198,564,399 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo ukarabati wa madarasa, ukamilishaji wa maboma ya madarasa, ujenzi wa nyumba za walimu.
Katika sekta hii Serikali ya awamu ya sita iliweza kujikita kwa vitendo kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata Elimu iliyo bora kwa kusomea katika mazingira ya kusomea na kujifunzia pamoja na kuhakikisha kuwa inapunguza umbali mrefu kwa wanafunzi kufuata shule.