Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
TAASISI ya UONGOZI inaandaa Kongamano la 8 la Kikanda la Viongozi wa Afrika linalotarajiwa kufanyika Aprili 7 – 8 mwaka 2025, jijini Kampala, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 5 Aprili 2025, Kongamano hili linaitishwa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ni Mlezi wa Kongamano na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Hailemariam Dessalegn Boshe, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia. Mada itakayojadiliwa ni “Kutimiza malengo ya maendeleo endelevu Afrika: Hatua zilizotekelezwa na mwelekeo wa baadaye”.
Washiriki wa Kongamano ni pamoja na Mhe. Dkt. Mohamed Moncef Marzouki, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Tunisia ; na Dkt. Ernest Bai Koroma, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Sierra Leone. Washiriki wengine ni viongozi waandamizi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika – na sekta zote ikiwemo sekta ya umma, sekta binafsi, sekta ya elimu ya juu, na sekta ya asasi za kiraia.
Kongamano hilo ni tukio muhimu litakalofanyika kabla ya Mkutano wa 11 wa Kikanda wa Maendeleo Endelevu wa Aprili 9 hadi Aprili 11 mwaka 2025, na unaoratibiwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi Barani Afrika(UNECA). Litajumuisha ufunguzi na mijadala itakayojikita kwenye mada kuu nne:
(i) Kutokomeza umaskini na kukuza uchumi;
(ii) Afya bora na ustawi;
(iii) Kuimarisha elimu na ujuzi; na
(iv) Mifumo madhubuti na endelevu ya kusimamia mazingira.
Lengo la Kongamano hilo kutoa fursa ya kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji, changamoto, na namna ya kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika. Malengo mahususi ni kujadili hatua zilizofikiwa na nchi za Afrika katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, kuainisha changamoto zinazokwamisha utekelezaji, kutengeneza mipango inayotekelezeka kwa ajili ya kutatua changamoto katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo kuhamasisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya nchi za Afrika, na kuleta mbinu zenye ubunifu na kuimarisha mashirikiano kwa ajili ya kuchochea maendeleo endelevu.
Kuhusu Taasisi ya UONGOZI: Taasisi ya Uongozi kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu Barani Afrika, maarufu kama Taasisi ya UONGOZI (UONGOZI Institute), ni taasisi ya kikanda ya kuimarisha kada ya uongozi iliyo chini ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taasisi hiyo lianzishwa mwaka 2010 na Serikali za Tanzania na Finland kwa lengo la ya kujenga na kuimarisha viongozi wa Afrika ili kukidhi matakwa ya ndani ya kutoa huduma kwa wananchi na kuyafikia maendeleo endelevu.
Pia taasisi inatambua kwamba sifa za uongozi hujengwa kwa namna endelevu. Hivyo, programu katika mihimili yake miwili – uongozi na maendeleo endelevu – zinatekelezwa kupitia maeneo makuu manne: Mafunzo ya uongozi, mijadala ya kisera, tafiti, na ushauri wa kitaalamu. Wateja wake ni pamoja na taasisi na watu binafsi kutoka kwenye sekta zote.