NA Vero Ignatus,Arusha
CHAMA cha wafawidhi wa matukio nchini Tanzania (KISIMA CHA MAFANIKIO ) wameandaa kongamano la kuongeza uelewa na maarifa kuhusu tasnia nzima ya ushehereshaji itakayoanyika jijini Arusha kuanzia Aprili 12 hadi Aprili 14 mwaka huu.
Kongamano hilo litafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) ambapo mgeni rasmi anatazamiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha Mwalim Bryceson Makena ambaye ni Muasisi wa Kisima cha Mafanikio amefafanua kongamano hilo la siku tatu litakuwa na zaidi ya washiriki 1000 ,ambapo lengo kuu likiwa ni kutoa mafunzo maalum ya ushehereshaji.
Amefafanua kuwa lengo ni kujenga ueledi katika shughuli za kiserikali ,sekta binafsi ,kijamii pamoja na shughuli za kisiasa na uratibu wa matukio yenye tija kwa taifa.
Amesema kwa kutambua juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na tatizo la ajira kwa vijana, kumomonyoko wa maadili na janga la kukosa uzalendo wao kama wadau wa tasnia husika wameamua kuunga juhudi hizo kwa vitendo.
Ameongeza watatumia nafasi yao kuelimisha ,kuhamasisha,kuburudisha ,kushauri pamoja na kujifunza sera ,miongozo,maelekezo,mipango mikakati na vipaumbele vya kitaifa kupitia majukwaa wanayowasiliana moja kwa moja na jamii kupitia shughuli wanazofanya.
“Chama chetu kina zaidi ya wanachama 450 waliogawanyika kanda 6,na bado tunaendelea kupokea wanachama wapya,mfawidhi wa matukio mmoja anaweza kukutana na watu zaidi ya 1000 kwa wiki katika matukio mawili tofauti ya muda wa kazi …
“Na baada ya kazi kwa mwezi anakutana na watu 4000.Fani hii inahitaji mafunzo rasmi na vyeti vya kitaalam tofauti na kauli zilizozoeleka mtaani kwamba vijana wengi wanaingia kwenye fani kwasababu ni kazi rahisi na mdomo haulipi VAT na hakuna gharama kubwa ya kuendesha kazi hii zaidi ya kuwa na suti tatu au nne,kitu ambacho kinashusha hadhi ,heshima,thamani ya taaluma’’alisema Makena.
Hivyo Makena ameiomba Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia namna ya kushirikiana nao ikiwemo Serikali itengeneze mfumo rasmi wa mafunzo ili kuleta tija na weledi katika tasnia.
“Serikali itumie wafawidhi matukio waliorasimishwa rasmi kisheria,kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).Pia BASATA wawashirikishe TAMISEMI kupitia viongozi wa serikali za mitaa katika kusimamia maadili ya tasnia kwa kupeleka muongozo sharia na kanuni za uendeshaji wa shughuli hizo.
Kwa upande wake Ester Kimweri ambaye ni Mwenyekiti wa Kisima cha Mafanikio amesema hadi sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 75 na kuongeza wameamua kufanya kongamano hilo Arusha ili wapate pia wasaa wa kwenda kutembelea vivutio vya utalii katika hifadhi za taifa.
‘’Sisi ni washehereshaji tutakapofika hifadhini kwanza kunachangia pato la Taifa ,pia tunayofursa ya kutangaza vivutio vilivyopo katika hifadhi zetu kwa kupitia kurasa zetu za kijamii,vilevile pale tunapopata wasaa tukiwa kwenye utendaji kazi wetu wa kila siku,”amesema Ester.
Akizungumza mmoja wa wanachama wa Kisima cha Mafanikio Happyness Mushi amesema kabla hajajiunga na chama hicho alikuwa ni mshehereshaji asiyejua namna ya kupangilia shughuli zake.
“Ilabaada ya kujiunga nimenufaika na elimu ambayo inatolewa mara kwa mara kwani nimejufunza namna bora ya kuratibu matukio katika shughuli za kijamii,kiserikali kwa kuzingatia itifaki.”
Kuhusu Kisima cha mafanikio ni chama kilichosajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2020 chini ya sheria ya Jumuiya ya 337 kwa usajili Na.SA 21669 ili kujishughulisha na nyanja za kitaaluma,kijamii kiuchumi na kitamaduni.
Pia kinatambuliwa na Wizara ya Habari ,Utamaduni Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Sanaa la Taifa kwa Sheria Na.23 ya mwaka 1984 na kupewa kibali cha kuendesha shughuli za Sanaa Nchini Na.BST-9684-190.
Mwl.Bryceson Makena ni muasisi wa Kisima amefafanua kuwa kongamano hilo la siku tatu litakuwa na zaidi ya washiriki 1000