Na Nihifadhi Abdulla Zanzibar:
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimeeleza faraja yake kufuatia uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutoa punguzo la ada kwa wanawake watakaochukua fomu za kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Akitoa taarifa hiyo Kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, amesema uamuzi wa ZEC ni wa kihistoria na unapaswa kupongezwa kwani umezingatia hali halisi ya kijamii na kiuchumi inayowakumba wanawake wengi Zanzibar
Amesema kupitia taarifa iliyosomwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC Redio) tarehe 10 Aprili 2025, imemnukuu Afisa wa ZEC akieleza kuwa punguzo hilo ni la nusu ya ada kwa wanawake wote wanaonuia kugombea nafasi mbalimbali. Hatua hii imelenga kuwahamasisha wanawake kushiriki zaidi kwenye nafasi za kisiasa na uongozi.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi Zanzibar katika ripoti ya uchaguzi wa mwaka 2020, kati ya wagombea 601 waliojitokeza kuchukua fomu, wanawake walikuwa 135 pekee – sawa na asilimia 22.4 ya wagombea wote. Idadi hiyo inaonesha uwakilishi mdogo wa wanawake kwenye siasa.
Aidha, katika uchaguzi huo, wanawake walioshinda nafasi kwa ushindani walikuwa 37 tu kati ya nafasi 160 za udiwani na uwakilishi, hali inayoonyesha pengo kubwa la ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za maamuzi.
TAMWA ZNZ imesema gharama kubwa zilizokuwepo hapo awali zilikuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wengi. Mfano, mgombea wa nafasi ya Udiwani alilazimika kulipa shilingi 10,000 kama ada, na dhamana ya 50,000. Kwa nafasi ya Uwakilishi, ada ilikuwa 50,000 huku dhamana ikiwa 300,000. Urais, ada yake ilikuwa 100,000 na dhamana ya milioni 2.
“Kwa niaba ya TAMWA ZNZ, napenda kupongeza uamuzi huu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ambao unaweka mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki katika siasa. Tunaamini kwamba kwa kupunguza ada ya kugombea, wanawake wengi zaidi watajitokeza kuchukua nafasi za uongozi. Huu ni wakati wa mabadiliko ya kweli na tunaendelea kuwahamasisha wanawake wote wenye sifa kuchangamkia fursa hii muhimu,” anasema Dkt. Mzuri Issa.
Kwa muktadha huo, uamuzi wa ZEC kupunguza nusu ya gharama hizo kwa wanawake unatazamwa kama hatua chanya itakayosaidia kuvunja vikwazo vya kiuchumi vinavyowakumba wanawake wengi, hasa wale walioko pembezoni.
TAMWA ZNZ imewataka wanawake wote wenye sifa, ari na uwezo wa uongozi, kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiandaa mapema kuchukua fomu na kugombea nafasi wanazohitaji katika uchaguzi wa mwaka huu.
Ripoti mbalimbali zimebainisha kuwa wanawake ni waathirika wakuu wa umasikini, huku wengi wao wakikosa mitaji, muda wa kushiriki siasa, pamoja na changamoto za majukumu ya kijamii na kazi zisizo na malipo majumbani.
Wakitoa maoni yao kufuatia uamuzi huo wa ZEC, baadhi ya wanawake wenye nia ya kugombea wameeleza matumaini na ari mpya waliyoipata. Bi mwanakhamis Haji, mkazi wa Kidimni anayetarajia kugombea amesema: “Kwa mara ya kwanza najihisi karibu na nafasi ya kuchukua uongozi. Punguzo hili linatoa matumaini mapya kwa wanawake kama sisi tuliokuwa tukiogopa gharama.”
Kwa upande wake, Maua Abdalla, mkaazi wa Koani ambaye awali aliwahi kugombea bila mafanikio mwaka 2020, amesema: “Nilishindwa kwa sababu ya vikwazo vya kifedha, lakini sasa najiandaa tena. Nafasi hii sitaiwacha.”
Wanawake wengi wameeleza kuwa hatua hiyo ni chachu ya mabadiliko katika usaw wa kijinsia kwenye uongozi wa Zanzibar, wakisisitiza haja ya jamii nzima kuwaunga mkono wanawake wanaojitokeza kugombea.