
Na Khadija Kalili , Michuzi TV
SHULE ya sekondari Mwambisi iliyopo Kongowe Wilayani Kibaha Mkoani Pwani imeibuka kidedea kwa asilimia 99 katika shindano la kupanda na kutunza miti Mashuleni lililoandaliwa na kudhaminiwa na Benki ya NMB nchini na kukabidhiwa hundi ya shilingi Mil.50 .
Akitoa taarifa ya hafla ya utoaji Zawadi kwa washindi wa kampeni ya upandaji miti nchini iliyofanyika Kibaha, Mkoani Pwani Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NMB Juma Kimori katika hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Mwambisi Kongowe ambapo Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohammed Mchengerwa alikuwa Mgeni rasmi.
Kimori amesema NMB ilitenga Milioni 225 kwaajili ya kufanikisha zoezi hilo lililohamasisha utunzaji wa mazingira kwenye shule za msingi na sekondari nchini ambapo kila shule iliyoshiriki shindano hilo ilikabidhiwa miche 2800 ya miti waipande na kuitumza ndipo Shule hiyo ya Sekondari Mwambisi imekuza miche yake kwa asilimia 99 na kufanikiwa kupata ushindi wa nafasi ya kwanza nchini.
Nafasi ya pili imechukuliwa na Shule ya Msingi Ibondo ya Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ambayo wamepata Mil. 30 na Shule ya Sekondari Itimbo ya Wilaya ya Mafinga Mkoani Iringa iliyopata Mil.20 imechukua nafasi ya tatu.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa akikabidhi hundi hizo amesema zoezi la upandaji miti na kutunza litakuwa ni moja ya kipimo cha utendaji kazi wa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa Wilaya nchini ikiwa pia ni kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais Dkt. Isdor Mpango kupanda miti milioni moja na nusu na kuitunza kwenye maeneo yao.
Aidha Mchengerwa amewapongeza Benki ya NMB kwa Kampeni ya miti na kusaidia serikali kutoa tuzo kwa washindi ambapo shule ya sekondari Mwambisi wameibuka washindi wa kwanza walipanda miti 1,800 na kuipanda yote.
“Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa kampeni ya upandaji miti nchini inakuwa endelevu, na kusisitiza utekelezaji wa jukumu hilo kwa ufanisi katika ngazi zote za uongozi kutokana na umuhimu wa hifadhi ya mazingira, viongozi wote wa serikali katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza maagizo hayo kwa vitendo, kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge, amesema miti Milioni 10 ilipandwa mwaka Jana Mkoani humo na kwa mwaka huu tayari imesambazwa jumla ya miche ya miti milioni kumi kwa ajili ya kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa Pwani.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa katika kutekeleza agizo la kitaifa la upandaji miti, ikiwa ni juhudi za kulinda mazingira na kuhakikisha Mkoa unakuwa na mazingira rafiki kwa maisha na maendeleo endelevu.