Na Diana Byera,Bukoba.
Timu ya wataalamu kutoka wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na waratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia wametoa mafunzo ya mwongozo wa kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Kagera watakaojitokeza kuwasilisha changamotoo zao za msaada wa kisheria.
Wataalamu walionufaika na mafunzo ya mwongozo na maafisa ustawi wa jamii,maafisa Maendeleo ya jamii ,maafisa Ardhi ,mawakili wa kujitegemea,maafisa wa Jamii kutoka madawati ya Polisi ,watakaokuwa kwenye kampeni hiyo ,watendaji wa kata zitakazotembelewa,wanasheria kutoka ngazi za Halmashauri zote za mkoa wa Kagera, lengo likiwa ni kupata uelewa wa pamoja wa kuhakikisha wananchi wanapata Haki ya kisheria bila kutumia Gharama yoyote katika ngazi zote za maamuzi .
Mkurugenzi wa kampeni ya msaada wa kisheria wa Mama Samia (MSLAC) Ester Msambazi akizungumza alisema kuwa anajivunia kuanzishwa kwa kampeni hiyo, kwani Kuna mafanikio makubwa sana tangu ilipoanzishwa Mei 2023 ikiwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro na kesi zilizodumu muda mrefu pamoja na wananchi kupata Elimu ya namna bora ya kuwasiliana na mawakili ili kufungua kesi zao.
“Tunapotoka hapa baada ya kupatiwa mafunzo ya miongozo ni lazima tuvue vyeo vyetu vyote,tuviweke pembeni tuwe kitu kimoja tufanye kazi kwa weledi tuwe wasikivu ,lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kutosha na kampeni hii inafanikiwa kufufua matumaini ya wananchi wanyonge ,kwa sababu wananchi wengi wanaokumbwa na changamoto hawana uwezo “amesema Msambazi
Amesema kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia inatarajia kutamatika Mei mwishoni mwaka huu na mara baada ya kampeni hiyo Kliniki za kutoa huduma za Kisheria bure Kila halmashauri zitafunguliwa na wananchi wanaendelea kupata Huduma huku mwananchi ambaye kesi yake haitapata utatuzi kwa siku tisa atapewa Wakili wa kumusimamia mpaka kesi yake imalizike.
Kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Kagera Issaya Tendega Amesema Kuwa mkoa wa Kagera unakumbwa na matatizo makubwa na inahitaji msaada wa kisheria katika Nyanga ya migogoro ya Ardhi,Mirathi na unyanyasi wa Kijinsia
Aidha Ametoa wito kuhakikisha wananchi wanaoishi vijiji vya pembezoni kupata msaada wa kisheria, kwani mara nyingi hawana nauli na gharama za kugharamikia kesi zao.
“Kama mkoa wa Kagera tutafurahi Kuona wananchi wetu migogoro inapungua kupitia kampeini hii, baadhi ya wananchi wanaogopa kusajili kesi zao kwa sababu ya gharama, hivyo uwepo wa kampeni hii ni Fursa kwa wananchi wote ,hivyo timu zilizopangwa zifanye kazi kwa weledi “amesema Tendega.