Na Mwandishi Wetu, Tanga
Ahadi ya Milioni Mbili iliyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM), Ummy Mwalimu, kwa Timu ya Coastal Union endapo itapata ushindi katika mchezo wao dhidi ya Singida Black Stars, imekuwa chachu ya kuchochea ushindi mara baaada ya kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja (2-1) katika mechi iliyochezwa Aprili 10, 2025, katika viwanja ya CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Ummy Mwalimu ambaye ni mdau mkubwa wa michezo mkoani Tanga, alipata wasaa wa kuongea na wachezaji wa Timu ya Coastal Union kabla ya mchezo huo.
Kimsingi, Ummy Mwalimu aliwasisitiza wachezaji hao kupambana kwa jasho na damu ili kupata ushindi huku akisisitiza kuwa atawakabidhi kitita cha Milioni Mbili mara baada ya kumalizika mchezo huo endapo wataibuka na alama tatu muhimu katika mchezo huo.
Kufuatia ushindi wa (2-1), Ummy Mwalimu alitimiza ahadi yake hiyo kwa kuwakabidhi wachezaji hao fedha taslimu Milioni Mbili, ambapo viongozi na wachezaji wa Coastal Union walimshukuru kwa kutimiza ahadi yake ambayo imewapa nguvu ya kupambana katika mchezo huo na katika michezo inayofuata pia.
Hii si mara ya kwanza kwa Ummy Mwalimu kuwaunga mkono Timu ya Coastal Union, amekuwa akifanya hivyo mara kadhaa kuhakikisha Timu hiyo inafanya vizuri ili kuuheshimisha mkoa wa Tanga kimichezo hasa katika mchezo wa mpira wa miguu.