Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Wanahabari, maarufu kama Samia Kalamu Awards.
Tuzo hizi zinalenga kuhamasisha uandishi wa habari za maendeleo kwa kufanya uchambuzi na utafiti wa kina, kuongeza maudhui ya ndani, kuzingatia weledi, maadili, uwajibikaji wa kitaaluma, kukuza uzalendo na kujenga taswira chanya ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Aprili 29, 2025 Jijini Dodoma, ambalo limeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema kuwa jumla ya washindi 79 watatunukiwa tuzo.
Amesema walengwa wa tuzo hizo ni waandishi wa habari, wachapishaji wa maudhui ya mtandaoni, maafisa habari, watangazaji pamoja na vyombo vya habari kwa ujumla.
Dkt. Reuben ameeleza kuwa tuzo hizo zimegawanywa katika makundi makuu matatu: tuzo maalumu za kitaifa, tuzo kwa vyombo vya habari, na tuzo za kisekta.
“Kundi la kwanza litahusisha Tuzo Maalumu za kitaifa ambazo ni pamoja na Tuzo ya chombo cha Habari Mahiri kitaifa, Tuzo ya wanahabari wabobevu, Tuzo ya afisa habari mahiri wa serikali, Tuzo ya mwandishi wa habari kitaifa na Tuzo ya uandishi wa Habari za matumizi ya nishati safi ya kupikia”
“Kundi la pili linajumuisha Tuzo kwa vyombo vya habari ambozo ni tuzo za Televisheni, Mtandaoni, Redio na Magazeti na Kundi la tatu tuzo za kisekta zinatolewa kwa waandishi wa habari waliobobea kuandika makala za maendeleo kwenye sekta mbalimbali. amesema Dkt Ruuben.
Aidha, ametoa wito kwa waandishi na vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha hafla hiyo ya kihistoria, inayotoa fursa kwa wanahabari kuonesha mchango wao kwa jamii na taifa kwa ujumla