Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amezindua rasmi malori saba ya kubebea mizigo yanayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 8 wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Liwale.
Katika tukio hilo, Dkt. Ndiege pia amekabidhi pikipiki tatu kwa AMCOS zilizofanya vizuri katika ulipaji wa malipo kwa wakulima wa wakati kwa AMCOS ya mbuyuni Liwale ,Ruangwa AMCOS na
Mtua AMCOS Nachingwea
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Ndiege amesisitiza kuwa Vyama vya Ushirika nchini vinapaswa kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili kwa njia endelevu.
“Mwaka jana RUNALI walikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, kutokana na ukosefu wa magari. Leo hii tunashuhudia uzinduzi wa malori haya saba ambayo yatakuwa msaada mkubwa kwa wakulima,” alisema Dkt. Ndiege.
Aidha, alibainisha kuwa malori hayo si tu yataongeza ufanisi katika kuhudumia wakulima kwa kusafirisha mazao kutoka kwa Vyama vya Msingi kwenda Chama Kikuu, bali pia yatakuwa chanzo kipya cha mapato kwa chama hicho, hivyo kupunguza utegemezi wa mapato kupitia ushuru pekee.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI, Bw. Odas Mpunga, alisema kuwa chama hicho kimejipanga kujiendesha kibiashara kwa kujenga hoteli kubwa katika Wilaya ya Liwale, hatua ambayo inalenga kuongeza vyanzo vya mapato.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Mhe. Mohammed Mtesa, alieleza kuwa ushirika ni njia muhimu ya kuwaunganisha watu na kwamba ni jukumu la wanachama kulinda mshikamano na kuepuka migawanyiko.
Aliongeza kuwa juhudi za bodi ya RUNALI kusimamia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati ni za kupongezwa. Pia alieleza kuwa ujenzi wa hoteli hiyo mpya utasaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa huduma za malazi wilayani humo.