
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisanga Stendi, Dotto Juma, amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na kushambuliwa kwa mapanga na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Aprili 15, 2025, katika Kata ya Tunuguo, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Tukio hilo linaelezwa kuibua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Dotto Juma alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine za mwili wake na kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambako anaendelea kupokea matibabu. Akizungumza akiwa hospitalini, Dotto ameeleza kuwa washambuliaji walivamia nyumbani kwake wakiwa na mapanga na walimshambulia wakimtuhumu kushindwa kusimamia kikamilifu migogoro ya mashamba inayodumu kijijini hapo.
“Walinivamia usiku wakiwa na silaha, walikuwa wakinituhumu kwa kushindwa kutoa suluhu kwenye mgogoro wa mashamba,” alisema kwa sauti dhaifu.
Daktari Noeli Kiboko kutoka Kitengo cha Magonjwa ya Dharura hospitalini hapo, amesema majeruhi huyo alipokelewa akiwa katika hali mbaya, lakini sasa hali yake imeanza kuimarika baada ya matibabu ya awali.
Mke wa mwenyekiti huyo alisimulia kwa huzuni jinsi walivyolazimika kupiga yowe kuomba msaada kutoka kwa majirani waliposikia kelele na harakati za ajabu nje ya nyumba yao usiku huo.
Kwa sasa jeshi la polisi mkoani Morogoro linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo, huku jamii ikihimizwa kujiepusha na kujichukulia sheria mkononi katika kushughulikia migogoro ya ardhi.