NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa amezindua Mfumo wa usimamizi na uendeshaji kazi za Sanaa AMIS ambao unaunganisha Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Taasisi nyingine hususani Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mfumo huo utarahisisha urasimishaji, kuongeza mapato pamoja na uendeshaji shughuli za Sanaa na kuweka kanzi data ya wasanii na wadau wa Sanaa.
Akizungumza leo Aprili 22, 2025 katika hafla hiyo na kufungua Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maendeleo ya Michezo kilichofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, amewataka Watanzania kuthamini na kulinda utamaduni wao kama msingi wa utambulisho wa taifa na urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha Majaliwa amesema utamaduni ni silaha muhimu ya kujenga mshikamano wa kitaifa na kukuza uchumi kupitia sanaa na michezo.
Ameeleza kuwa mageuzi ya kisayansi na kiteknolojia duniani yameleta muingiliano mkubwa wa tamaduni, hivyo kuna haja ya kuwa makini ili mabadiliko hayo yapelekee mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watanzania hasa vijana huku akiwataka Maafisa wa sekta hizo kuhakikisha kuwa msingi wa utamaduni wa taifa unaenziwa, unalindwa, na unarithishwa ipasavyo.
“Kamwe tusikubali kukumbatia tamaduni zinazokwenda kinyume na maadili na ustaarabu wetu. Tusikubali kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni ambazo zinadhalilisha utu wetu. Pamoja na umuhimu wa kujifunza mambo mazuri ya tamaduni nyingine ni lazima kuchuja nini cha kuchukua na nini cha kuacha.” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzipa kipaumbele sekta za utamaduni, Sanaa na michezo na hivyo kuziwesha kuwa na mafanikio makubwa. “Michezo ina nguvu na ushawishi mkubwa katika kuleta maendeleo na miongoni mwa michezo inayoongoza kuliletea Taifa fedha nyingi za kigeni ni riadha.”
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Mchezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta.

Awali, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Hamisi Mwinjuma amesema kuwa ili kuendelea kuvutia mageuzi ya kidijitall, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imefanikisha uunganishaji wa Mfumo wa Wadau wa Sanaa (AMIS) na Mfumo wa TAUSI. Ametolea mfano mapato ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) yameongezeka kwa asilimia 200 kutokana na kuunganishwa kwa mifumo hiyo ya makusanyo.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa Kikao kazi hicho ni cha kimkakati katika kuleta mabadiliko makubwa kwa sekta za utamaduni, sanaa na michezo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita.