Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Balozi Omar Ramadhani Mapuri ameongoza kikao cha pamoja kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wadau wa uchaguzi wa Jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Temeke ikiwa ni kujiridhirisha juu ya taarifa zilizotumwa wakati wa maombi ya kuligawa jimbo la Ukonga lililopo katika jiji la Dar es Salaam na Jimbo la Mbagala lililopo katika Manispaa ya Temeke.
Awali akifungua kikao hicho, Mhe.Balozi Mapuri alisema kuwa moja kati ya majukumu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 75(4) na 74(6)(c) ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1) (d) cha sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.1 ya mwaka 2024 ni kuchunguza na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika majimbo ya uchaguzi, hivyo kikao hicho kinafanyika kwa mujibu wa sheria.
“Tume imechagua kutembelea baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ni sahihi kuhusu jimbo husika, aidha ibara ya 75(3) na (4) imeainisha vigezo vya ugawaji wa majimbo ambavyo ni idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano, hali ya kijiografia, hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya Wilaya au Halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya muungano, uwezo wa ukumbi wa Bunge; na idadi ya viti maalum vya wanawake. Vigezo vingine vinavyozingatiwa na Tume katika kugawa majimbo vimeainishwa katika Jedwali la Tatu la Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024,”alisema Balozi Mapuri.
Miongoni mwa waliohudhuria vikao hivyo ni pamoja na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Viongozi wa Vyama vya Siasa mkoa wa Dar es Salaam, Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake, vijana, wenye ulemavu na wazee wa Kimila.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipokea mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.