Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waziri wa Madini Mhe Anthony Peter Mavunde ametoa Rai kwa Wawekezaji wote kwenye Sekta ya Madini Nchini kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini,Sura 123 na kuahidi Wizara hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao.
Waziri Mavunde ameyasema hayo mapema Leo hii Jijini Dodoma Aprili 23,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akimpongeza Dkt Samia,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024.
“Naomba nitoe Rai kwa wawekezaji wote kwenye Sekta ya Madini kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura 123. Wizara ya Madini itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na kukuza uchumi wa Taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini”.
Aidha Waziri ameeleza kuwa Sekta ya Madini nchini Tanzania imepiga hatua kubwa ya kihistoria kwa kufikia mchango wa asilimia 10.1 katika Pato la Taifa mwaka 2024, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya lengo lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026).
“Ni jambo la kujivunia kuona kuwa juhudi za Serikali na wadau wa sekta hii zimezaa matunda. Mwaka 2023 tulikuwa na mchango wa asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa. Leo hii, tunazungumza kuhusu ongezeko hadi asilimia 10.1 kwa mwaka 2024. Hili si jambo dogo”.
Waziri Mavunde amesema kuwa, Mafanikio hayo yametokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria yaliyofanyika katika Sekta ya Madini tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Ametaja miongoni mwa hatua zilizo changia mafanikio hayo kuwa ni pamoja na: Kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli ya Serikali kupitia sekta hiyo, Kuanzishwa kwa minada ya madini ya vito, Udhibiti wa utoroshwaji wa madini, Kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, pamoja na Kuanza kwa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo pia kuwashukuru wadau wote wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo pamoja na wahusika wote waliopo kwenye mnyororo mzima wa sekta ya Madini , watendaji wote wa sekta na taasisi zake kwa ushirikiano mzuri na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ambao umekuwa na matokeo chanya.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mafanikio hayo yameonesha wazi kuwa Sekta ya Madini si tu kichocheo cha ukuaji wa uchumi bali ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni, ajira, na maendeleo ya kijamii kwa Watanzania.