Na Issa Mwadangala
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga akiwa ameambatana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Songwe Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Maria Kway pamoja na wafanyakazi waandamizi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini Mamba Bi.Mary Dancan na Chediel Mshana ambao ni mameneja wa Mgodi huo Aprili 24, 2025 amefanya ukaguzi wa mradi wa kituo cha Polisi Ngwala kilichojengwa Kata ya Ngwala Wilaya na Mkoa wa Songwe ambacho kinatarajiwa kuwekwa jiwe la Msingi na Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde Aprili 28, 2025.
Mradi huo unajengwa na kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na samani zote za kituo hicho. Akiwa katika kituo hicho Kamanda Senga ameipongeza Kampuni hiyo kwa hatua waliofikia za umaliziaji (finishing) na kusema kuwa kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kata hiyo na maeneo jirani.
Kwa upande wake Maneja wa Mgodi huo, Mary Dancan alisema kuwa lengo la kujenga kituo hicho ni kuendeleza ushirikiano na taasisi za Serikali kwa ajili ya kufikisha huduma kwa jamii hasa katika masuala ya elimu, afya na usalama ili jamii iendelee kuwa salama katika uchumi wa bluu.