Farida Mangube, Morogoro
Katika juhudi za kupambana na changamoto ya ajira kwa vijana na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi nchini, Chuo Kikuu Mzumbe kimeandaa kongamano la siku tatu lenye lengo la kukuza ujasiriamali na ubunifu miongoni mwa wanafunzi.
Kongamano hilo litakalofanyika kuanzia Mei 7 hadi Mei 9 mwaka huu, litawakutanisha wanafunzi wabunifu, wahitimu wa chuo hicho, wafanyakazi wa Mzumbe, makampuni binafsi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Uhusiano wa Kitasnia, Prof. Emmanuel Chao alisema kuwa tukio hilo linalofanyika kila mwaka tangu 2017, linalenga kuonesha mchango wa chuo hicho katika kushughulikia changamoto ya ajira kupitia ubunifu na elimu ya vitendo.
“Tumekuwa na tukio hili la Siku ya Mzumbe tangu mwaka 2017 ambapo tunawaleta pamoja wanafunzi wetu, wahitimu na wadau mbalimbali ili kuonesha ubunifu unaofanyika chuoni na jinsi unavyoweza kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema Prof. Chao.
Aliongeza kuwa katika siku hizo tatu kutatolewa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo huduma za afya, biashara na teknolojia, sambamba na maonesho ya bidhaa na miradi ya ubunifu kutoka kwa wanafunzi wa Mzumbe.
Kwa mujibu wa ratiba, siku ya kwanza ya kongamano itahusisha utoaji wa huduma za kijamii pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, huku pia kukifanyika chakula cha pamoja kwa wadau na wahitimu wa chuo hicho. Siku ya pili itahusisha maonesho ya wajasiriamali na wabunifu, na siku ya mwisho kutakuwa na mashindano ya ubunifu, mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu pamoja na uzinduzi wa bidhaa mpya zilizobuniwa na wanafunzi.
Prof. Chao alibainisha kuwa washindi wa mashindano hayo watapata fursa ya kuunganishwa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya uwezeshaji na kukuza miradi yao.
“Tunataka kuona vijana wetu wakipata fursa ya kuendeleza mawazo yao ya kibunifu na hatimaye kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira nchini,” alisisitiza Prof. Chao.