Na Belinda Joseph, Songea – Ruvuma
Wazazi na walezi wametakiwa kuongeza ushirikiano wao katika malezi na ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto wao shuleni, kwani jukumu la mzazi halikomi kwa kulipa ada pekee, bali linahusisha pia kujua mwenendo na tabia ya mtoto katika mazingira ya shule na jamii.
Wito huo umetolewa na Mshauri wa Jeshi la Akiba Mkoa wa Ruvuma, Kanali Charles Christopher Mzena, kwa niaba ya Brigedi Kamanda Meja Jenerali Charles Peter Feruzi, wakati wa mahafali ya 20 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Ruhuwiko, inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kanali Mzena amesema kuwa baadhi ya wazazi hujihusisha zaidi na kutoa fedha kwa watoto wao pasipo kujua changamoto na mahitaji halisi ya kitabia na kitaaluma wanayokumbana nayo. Ameeleza kuwa, “Mtoto kwa mzazi hakui,” hivyo ni muhimu wazazi kuendelea kutoa mwelekeo wa maisha, maadili, na nidhamu hata baada ya watoto wao kufika hatua ya kidato cha sita.
Aidha, alikemea vikali tabia zisizofaa ambazo zinashamiri mitaani kama matumizi ya dawa za kulevya, bangi, na mienendo mingine isiyofaa, akisisitiza kuwa vijana bado wanahitaji uangalizi mkubwa na maelekezo ya karibu kutoka kwa wazazi ili kuwasaidia kuwa raia wema wenye mchango chanya kwa taifa.
Katika nasaha zake kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo, aliwataka kuiga mifano mizuri ya watangulizi wao na kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao. Alisisitiza umuhimu wa wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu kwa ajili ya mafanikio ya pamoja ya wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ruhuwiko, Luteni Kanali Benedicto Simon Bahame, alieleza mafanikio ya shule hiyo tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni pamoja na kupata tuzo mbalimbali, barua za pongezi, na kutajwa kuwa shule inayoongoza kwa ufaulu miongoni mwa shule 10 za JWTZ.
Aidha, alieleza kuhusu mchango wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacobo Mkunda, ambaye mnamo Novemba 2022 alitembelea shule hiyo na kuchangia kiasi cha shilingi milioni 238 kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi mkubwa wa kisasa ambao sasa umeanza kutumika.
Wakati huo huo, Mhitimu wa Kidato cha sita Omary Ramadhan, akisoma risala ya wahitimu, alielezea mafanikio waliyoyapata kipindi chote cha masomo, ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu kutokana na mpango wa kuhamishia wanafunzi wote wa kidato cha sita kwenye mabweni ili kuwawezesha kujisomea kwa utulivu. Pia walishiriki kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo michezo, utalii, na kuanzisha vilabu vya dini, TRA, na TAKUKURU, ambavyo vimewajengea uwezo mkubwa wa kiujuzi na kijamii.
Mwakilishi wa Bodi ya shule hiyo aliwatakia wanafunzi mtihani mwema, huku akiwakumbusha kuendelea kudumisha maadili waliyofundishwa, akisema kuwa “elimu bila nidhamu si lolote.”
Kwa sasa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,155, ambapo wahitimu wa kidato cha sita ni 274, wakiwemo wasichana 84 na wavulana 190. Aidha, ina jumla ya watumishi 159, wakiwemo walimu wanajeshi 45 na walimu wa kawaida 83. Inafundisha tahasusi za Sayansi, Sanaa, na Biashara, huku matarajio ya mwaka huu yakiwa ni kuongeza tahasusi mpya na kufaulisha wanafunzi wote kwa daraja A.