MKuu wa Wilaya ya Ubungo Mh. Lazaro Twange amemuagiza Mkuu wa Polisi, Wilaya ya Kipolisi Kimara/Ubungo kuwatafuta na kuwakamata watu wote waliovamia na kuchoma moto Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Msewe, na kuteketeza Nyaraka na Samani zote za Ofisi hiyo.
Tukio hilo la kuvamia na kuchoma moto ofisi hiyo limetokea majira ya saa 5 na nusu usiku wa kuamkia April 26, 2025 ambapo nyaraka na samani zote zikiwemo Viti na Meza zimeteketea.
Baadhi ya mashuhuda wameeleza kuwa walishuhudia moto ukiwaka katika ofisi hiyo na hivyo kuanza juhudi za kuokoa samani na kuzima moto.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Ubungo Bi. Elizabeth Erick amesema wahalifu hao kabla ya kuchoma moto jengo hilo waliiba meza na viti vipya vyenye thamani ya shilingi laki 4 na nusu.
Kufuatia tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ikiongonzwa na Mkuu wa Wilaya ilifika na kujionea madhara yaliyotokea, ambapo amesema kilichofanyika ni uvunjifu wa amani sambamba na kulitaka jeshi la polisi kuwasaka wahusika.
Pamoja na Mambo mengine, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo ambaye ndiye Diwani wa Kata ya Ubungo Mh. Jaffar Nyaigesha amewataka wananchi na Ofisi ya Mkurugenzi kushirikiana na vyombo vya usalama, kuweka ulinzi wa kutosha katika ofisi zote za Serikali.
Akizungumza baada ya kupokea maelekezo ya kamati ya ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Bi. Kissa Mbilla amewahakikishia wananchi kuwa ndani ya siku saba ofisi hiyo itakarabatiwa na kurejesha huduma za kijamii kama zilivyokuwa awali.