Katika kuadhimisha Wiki ya Usalama Mahala pa Kazi, kampuni ya GASCO imeendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi salama na nafuu ya gesi asilia, hasa kwenye vyombo vya moto.
Katika banda la GASCO, wananchi walijitokeza kwa wingi kujifunza zaidi kuhusu teknolojia ya kutumia Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) kama mbadala wa mafuta ya petroli na dizeli.
Akizungumza mbele ya wageni mbalimbali waliotembelea banda hilo, Mhandisi Hassan Temba alifafanua faida nyingi za matumizi ya gesi asilia kwenye magari ikiwemo kuokoa gharama.
“Gesi asilia ni salama zaidi kwa mazingira, inapunguza gharama za uendeshaji wa magari kwa zaidi ya asilimia 50, na inapunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa mazingira,” alisema Temba.
Aidha Temba, alisisitiza kuwa usalama wa matumizi ya gesi asilia umepewa kipaumbele, ambapo magari yanayofungwa mifumo ya gesi hupitia taratibu za ukaguzi wa kina na zinazozinggatia viwango vya juu vya usalama vya kitaifa na kimataifa.
Mhandisi Temba akitoa ufafanuzi wa matumizi ya gesi kwenye magari kwa wannachi waliotembelea banda la GASCO
Wananchi wamehimizwa kutokuwa na hofu juu ya upatikanaji wa gesi asilia kwa magari yao, kwani TPDC imejipanga vizuri kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa uhakika ikiwa ni pamoja na kushirikisha sekta binafsi na taasisi nyingine ili kupanua mtandao wa vituo vya kujaza gesi nchini.
Katika hatua muhimu ya kuendeleza matumizi ya nishati safi na salama nchini, Afisa Maendeleo ya jamii Bw. Oscar Mwakasege ameeleza kuwa TPDC imekamilisha ujenzi wa kituo mama cha gesi asilia eneo la Chuo kikuu Dar es salaam kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya vyombo vya moto.
‘‘Kituo hiki kitaongeza unafuu kwa watumiaji hali itakayochochoea kukua kwa uchumi na kuongeza tija kwa wananchi katika sekta ya usafirishaji.
Kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia magari zaidi ya 1000 kwa siku na kusambaza bidhaa hiyo kwa vituo vingine ni dhahiri kitasaidia kupunguza kero waliyokuwa wanapata watumiaji wa vyombo vya moto. Ujenzi wa kituo hiki ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi asilia kama mbadala wa nishati ya mafuta. Alisema Oscar.