SHERIA ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, haijatoa fursa ya kuwafikiria Waandishi wa Habari au watu wanaofanya kazi za kihabari, bila kukidhi vigezo vya kielemu hususan kiwango cha chini cha Astashahada ya Uandishi wa Habari (Diploma) kutoka Vyuo vya Uandishi wa Habari vinavyotambulika.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 28 Aprili, 2025 na Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Mgaya Kingoba wakati akijibu swali la mmoja wa watangazaji wa Radio Tumaini Bruno Bomola aliyetaka kujua, Bodi hiyo inawafikiriaje wale wanaofanya kazi za kihabari bila kuwa na kiwango kilichotajwa katika Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari.
“Sheria haijasema tumfikiriaje mtu huyo, Sheria imesema Kiwango cha kuanzia ni diploma ya uandishi wa habari, kwa hiyo kama huna Diploma hutaruhusiwa kufanya kazi za kihabari ndani ya nchi hii, na ina maana unatakiwa ukasome au utafute utaratibu mwingine,” amesema Kingoba.
Bw. Kingoba amesema Sheria imeipa Bodi mamlaka ya kutoa Ithibati, Vitambulisho, kutunza kumbukumbu za Orodha ya Waandishi wa Habari na pia kushirikiana na wadau wakiwemo Waajiri/ wamiliki wa vyombo vya Habari na Vyuo vinavyotoa taaluma, hivyo itakuwa rahisi kufuatilia na kuwatambua wasio na sifa.
“Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi Wakili Patrick Kipangula, mwishoni mwa mwezi huu Aprili au mwanzoni mwa Mei 2025, mfumo wa Usajili Waandishi wa Habari utakuwa umekamilika na tutaanza kufanya usajili na kutoa vitambulisho kidijitali na tutatangaza. Haitakuwa tena kujaza fomu za karatasi badala yake waandishi watajaza fomu kwenye mfumo na kila kitu kitafanyika kidijitali”, amesisitiza.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, iliyotangazwa Septemba, 2024 ni chombo cha kitaaluma, kilichoundwa chini ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229, kifungu cha 11, chenye jukumu la kukuza taaluma ya Uandishi wa Habari.