Na Mwandishi Wetu – Songea
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoa wa Ruvuma, MNEC Hemed Challe, amewataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kuendelea kuhamasisha ulipaji wa ada ya uanachama, akisema kuwa hilo ni jambo la msingi katika kuimarisha uhai wa chama na kujipanga kwa ushindi mnono katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza Aprili 28, 2025, wakati wa kufunga ziara yake ya siku tatu katika Manispaa ya Songea, alisema kuwa chama chochote cha siasa kinahitaji kuwa na wanachama hai, wanaoshiriki katika shughuli za chama ikiwa ni pamoja na ulipaji wa ada ambao ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya chama.
“Uhai wa chama uko mikononi mwa wanachama wake. Tukilipa ada kwa wakati, tunakijengea chama uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya kisiasa kwa ufanisi,” alisema MNEC Challe mbele ya mamia ya wanachama waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Songea.
Katika ziara yake iliyoanzia Wilaya ya Nyasa, kisha Mbinga na hatimaye Songea Mjini, amesema ameshuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya uboreshaji wa huduma kwa wananchi.
“Tumejionea kwa macho namna fedha nyingi zimeelekezwa kwenye miradi ya barabara, afya, elimu, maji na nyinginezo Serikali ya CCM inatekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi,” aliongeza.
Akiangazia uchaguzi mkuu ujao, MNEC Hemed alisema kuwa mwaka huu ni wa kipekee kwa Mkoa wa Ruvuma umepata heshima ya kutoa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi Hivyo, aliwataka wananchi wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wanampigia kura nyingi Rais Samia Suluhu Hassan na kuvunja rekodi ya kitaifa ya kura za urais.
“ Mwaka 2015 mkoa aliotoka Rais Samia uliongoza kwa kupata kura nyingi za urais kutokana na kuteuliwa kuwa mgombea mwenza , lakini mwaka huu ni zamu yetu twende tukavunje rekodi kwa heshima ya Dkt. Nchimbi, ambaye ni mgombea mwenza wa Rais,” alisema kwa msisitizo.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa mikutano ya hadhara katika kata tano za Matogoro, Mateka, Seedfarm, Ndilimalitembo na Mletele ambazo zilikutana kwenye ukumbi wa chuo cha Ualimu Songea, kabla ya kumalizia katika Kata ya Mshangano, ambapo wanachama na wananchi kutoka kata jirani walihudhuria kwa wingi.
Viongozi mbalimbali wa chama walitumia jukwaa hilo kutoa taarifa za utekelezaji wa ilani ya CCM na kupokea maoni, changamoto na mapendekezo kutoka kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu.