Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Katika jitihada za kukabili changamoto za ununuzi wa Umma, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendelea na zoezi la kuwajengea uwezo wazabuni juu ya matumizi ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST).
Akifungua mafunzo ya siku mbili (tarehe 29 – 30 Aprili, 2025) kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika jijini Mbeya, Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amewataka wadau wa ununuzi wa umma kujifunza kuhusu moduli hiyo vizuri ili kuwawezesha kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha.
“Ili kuendana na matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 pamoja na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za mwaka 2025, PPAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetengeneza Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST),” alisema Bw. Sando
Bw. Sando aliongeza kuwa, moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki inafaida nyingi kwa wazabuni, taasisi nunuzi na PPAA kwa kuwa inarahisisha zoezi la uwasilishaji na ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.
“Moduli hii ina faida mbalimbali zikiwemo, mzabuni kutolazimika kufika katika ofisi za taasisi nunuzi au za PPAA ili kuwasilisha lalamiko au rufaa yake, kupunguza gharama na muda kwa wazabuni wakati wa kuwasilisha malalamiko au rufaa pamoja na kuongeza uwazi katika mchakato wa ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa,” aliongeza Bw. Sando.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando aliongeza kuwa hadi kufikia mwezi Aprili 2025, PPAA imeweza kushughulikia mashauri 185 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya Ununuzi wa Umma. Aidha, katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 36 wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika. Hatua hii iliepusha Serikali kuingia katika mikataba ambayo ingepelekea kuwa na utekelezaji wa miradi usioridhisha hivyo kusababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kaminishna Msaidizi Idara ya Sera ya Ununuzi na Ugavi, Wizara ya Fedha, Bi. Emma Komba aliwahimiza washiriki kutumia fursa ya mafunzo hayo kujifunza namna ya uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki kupitia moduli hiyo ili kuweza kuleta tija katika ununuzi wa umma.
Mafunzo kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni muendelezo wa mafunzo yaliyofanyika katika Kanda ya Pwani iliyojumuisha washiriki kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro; Kanda ya Ziwa iliyojumuisha washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga, Mara na Kagera pamoja na Kanda ya Kaskazini iliyojumuisha washiriki kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando akiongea na wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST). Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Mbeya kwa mikoa ya Nyanda za Juu kusini.
Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando akiongea na wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST). Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Mbeya kwa mikoa ya Nyanda za Juu kusini.

Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA, Bi. Florida Mapunda akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya
Kaminishna Msaidizi Idara ya Sera ya Ununuzi na Ugavi, Wizara ya Fedha, Bi. Emma Komba akiongea na washiriki kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma
Sehemu ya washiriki wakifuatilia mafunzo kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya