Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma imewataka waajiri katika taasisi mbalimbali kuhakikisha hawawazuii wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi, kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kutetea maslahi yao.
Wito huo umetolewa leo Mei 1, 2025, na Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma Nicodemus Mwakilembe, leo katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Kimkoa katika Uwanja wa Majimaji Mjini Songea.
Mwakilembe amesema kuwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ni haki ya kila mfanyakazi na ni njia halali ya kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea na kudai haki na maslahi yao kazini, amebainisha kuwa wako katika mchakato wa kujiunga na Chama cha Wafanyakazi na wakusanya kodi Tanzania (TAREWU), hatua ambayo itawezesha wafanyakazi wa taasisi hiyo kushiriki kikamilifu katika harakati za vyama vya wafanyakazi.
“Ni muhimu waajiri wakatambua kuwa kuwaruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi si upendeleo bali ni haki yao kisheria. Vyama hivi vina nafasi kubwa katika kusaidia kutatua changamoto za kiutumishi na kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi,” alisema Mwakilembe.
Katika hotuba yake, amewahimiza wafanyakazi kuendelea kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa moyo licha ya changamoto mbalimbali, akisisitiza kwamba kutimiza wajibu ni msingi mzuri wa kuwawezesha kudai haki zao kwa ufanisi.
Aidha, Mwakilembe amewakumbusha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, amesema kuwa kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, kwani ndizo zinazoendesha shughuli muhimu za serikali kama ujenzi wa shule, hospitali, barabara na huduma nyingine za kijamii.
Amehimiza pia matumizi sahihi ya mashine za EFD kwa wafanyabiashara kwa kutoa risiti kila wanapouza bidhaa, huku akiwaasa wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa, kwani kila Mtanzania ana jukumu la kushiriki katika ujenzi wa taifa kupitia ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.
Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika chini ya kauli mbiu: “Uchaguzi Mkuu wa 2025 utuletee viongozi wanaojali na kuthamini haki na maslahi ya wafanyakazi, sote tushiriki.”