Bajeti ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha
2025/26 imewasilishwa rasmi bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango
na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa
shughuli za wizara hiyo pamoja na taasisi zilizo chini yake kama vile Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).
Mara baada ya kuwasilishwa, wadau mbalimbali wa maendeleo na
masuala ya kijamii wamekuwa wakitoa maoni yao kuhusu bajeti hiyo, wakisisitiza
umuhimu wa kujumuisha mahitaji ya makundi yote ya kijamii, hususan wanawake na
vijana.
Ocheki Msuva, Mkurugenzi wa Shirika la Bridge for Change, ni
miongoni mwa wadau waliopitia bajeti hiyo kwa karibu. Akitoa maoni yake, Bw.
Msuva amesema bado kuna changamoto ya ujumuishaji wa jinsia, ambapo miradi
mingi ya uwekezaji huonekana kuwanufaisha zaidi wanaume.
“Kuna haja ya kupitia upya Dira ya Taifa ili miradi ya
uwekezaji tunayoiweka iguse makundi yote ya kijamii. Ajira nyingi zinazotokana
na miradi hiyo zinaelekezwa kwa wanaume, hali inayowatenga wanawake katika
maendeleo ya taifa lao,” amesema Bw. Msuva.
Naye mwanaharakati wa masuala ya kijinsia, Kenneth Anjelita,
ameitaka serikali kuhakikisha kuwa bajeti zake zina uhalisia unaoweza kuonekana
moja kwa moja katika maisha ya wananchi wa kawaida.
“Bajeti inapaswa kuwa chombo halisi cha maendeleo.
Wananchi wanataka kuona mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha yao ya kila
siku. Hii ni pamoja na huduma bora za afya, hasa kwa wanawake na watoto walioko
maeneo ya vijijini ambako huduma hizo bado ni changamoto,” amesema
Kenneth.
Wadau hao wametoa rai kwa serikali kuendelea kusikiliza
maoni ya wananchi wakati wa mchakato wa kuandaa na kutekeleza bajeti.
Wamesisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti kwa ufanisi ndio kipimo halisi cha
mafanikio ya mipango ya maendeleo ya taifa.
Kwa ujumla, bajeti ya 2025/26 imeonekana kuwa na malengo
makubwa ya kukuza uwekezaji nchini, lakini wadau wanashauri kuwa mafanikio yake
yatategemea namna ambavyo itatekelezwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, uwazi
na ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua.