
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ametoa kauli kali ya kulaani tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, huku akilielekeza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumhoji mtu aliyetoa kauli ya vitisho mitandaoni dhidi ya kiongozi huyo wa dini.
Katika tamko lake, Waziri Bashungwa amesema:
“Naliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta kwa haraka yule mtu aliyeandika mitandaoni kwamba ‘siku za Kitima zinahesabika’. Ahojiwe, ametumwa na nani, na hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika.”
Amesema tukio hilo linakiuka misingi ya amani na mshikamano wa kijamii ambao viongozi wa dini wamekuwa wakilinda kwa miaka mingi. Aidha, Serikali imesema inaendelea kuthamini mchango wa viongozi wa dini katika kulijenga taifa kwa misingi ya maadili na mshikamano.
MAAGIZO MENGINE YA BASHUNGWA:
- Jeshi la Polisi pia limeagizwa kuwatafuta wote waliohusika kutengeneza na kusambaza waraka feki uliodaiwa kutolewa na TEC.
- Waraka huo umetajwa kuwa na malengo ya kuchochea uhasama kati ya Serikali na Kanisa, jambo ambalo Serikali imesema halikubaliki.
Serikali imeeleza masikitiko yake na kumtakia Padre Dkt. Kitima uponaji wa haraka, huku ikisisitiza kuwa haki itatendeka kwa wote waliopanga au kushiriki katika shambulio hilo la kikatili.