Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ruvuma limewataka wananchi kupuuza uvumi kuwa magari ya zimamoto hufika kwenye matukio bila maji, na kusisitiza kuwa magari hayo huandaliwa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto.
Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Ruvuma, Melania B. Nyabwinyo, alitoa ufafanuzi huo wakati wa bonanza maalum kwa watumishi wa jeshi hilo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Zimamoto, Alisisitiza kuwa magari ya zimamoto huondoka yakiwa na vifaa vyote muhimu vikiwemo maji na vifaa vya uokoaji.
“Si kweli kwamba magari yetu hufika bila maji. Tunazingatia maandalizi yote muhimu kabla ya kwenda kwenye tukio,” alisema Kamanda Nyabwinyo.
Aidha, Kamanda aliwahimiza askari wa zimamoto kuepuka uadui na wananchi na badala yake kushirikiana nao kwa karibu, akisema wanapaswa kuwa watumishi wa jamii na si kinyume chake.
Katika hatua nyingine, alitoa pongezi kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Menejimenti kwa kuwathamini askari wa Ruvuma kwa kuwapandisha vyeo. Askari waliopandishwa walivalishwa vyeo rasmi mapema leo na kupewa wito wa kuendelea kuchapa kazi kwa bidii.
Pia, Kamanda Nyabwinyo aliwaalika wananchi kushiriki kilele cha Wiki ya Zimamoto kitakachofanyika Mei 4, 2025, katika viwanja vya Stendi ya Mfaranyaki, ambako elimu kuhusu huduma za zimamoto itatolewa na maswali ya wananchi kujibiwa moja kwa moja.
Maadhimisho haya hufanyika kimataifa kwa kuwakumbuka askari wa zimamoto waliopoteza maisha wakiwa kazini, wakiwemo watano waliokufa katika moto wa msitu jimbo la Victoria, Australia. Kamanda alisisitiza umuhimu wa mazoezi na maandalizi ya mara kwa mara ili kuongeza ufanisi wa huduma za uokoaji.