Mwandishi Wetu-Denmark
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amefanya mkutano wa kimkakati wa uwili (Bilateral Meeting) kati ya Tanzania na Viongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (Europian Union).
Katika Mkutano huo uliofanyika Mei 8, 2025 jijini Copenhagen, Denmark Waziri Masauni ameelezea mkakati wa Tanzania katika utekelezaji wa programu za Mabadiliko ya Tabianchini.
Mkutano huo umehudhiriwa na viongozi wakuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya akiwepo Bw. Wopke HOEKSTRA Kamishna wa Mazingira wa Ulaya, Bw. Krzysztof Bolesta, ambaye ni Katibu wa Nchi Wizara ya Hali ya Hewa na Mazingira- Poland akimwakilisha Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya pamoja na Bw. Christian Stenberg, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Hali ya Hewa/ Mazingira, Nishati na Fedha.
Katika Mkutano huo Mhe. Masauni aliambatana na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala ya Mazingira na mabadiliko ya Tabianchi Dkt. Richard Muyungi, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Pamoja na masuala ya kubadilishana mawazo kuhusu vipaumbele kabla ya vikao vya Bonn na COP30, na Mwelekeo wa Nchi za kiafrika ambapo Tanzania ni mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN).
Waziri Masauni alieleza kuhusu vipaumbele vitatu vya Tanzania ambavyo ni kuendelea kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia njia mbalimbali vikiwamo vitu vya asili; kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa watanzania kutumia nishati safi ya kupikia hadi kufikia kiwango cha asilimia 80 ifikapo mwaka 2034na kuendelea kuzijengea uwezo Taasisi zinazoratibu masuala ya biashara ya kaboni nchini.
Mhe. Masauni amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Umoja huo wa Ulaya kuangalia namna bora ya kuiwezesha katika masuala ya kujengea uwezo, misaada ya kifedha yenye masharti nafuu, ruzuku na Teknolojia ya upimaji wa kiwango cha kaboni.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Sasa wa EU, Bw. Krzysztof Bolesta, ameipongeza Tanzania kwa namna ilivyochukua hatua za kuanzisha Kituo cha Kaboni ambacho ni cha mfano kwa nchi za Afrika.
Aidha, alieleza kuwa siku zote Umoja wa Ulaya umekuwa ukifanya kazi na kuongoza kwa mfano mzuri na kwa kudumisha uwazi na haki na hivyo itaendelea kuhakikisha inatenda haki ya kutimiza ahadi zake zote za ufadhili wa programu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini.