Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga
Jamani eeeh! Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni mtu bingwa wa huduma za maji nchini. Pamoja na kwamba, serikali yake inafanya kazi usiku na mchana kuboresha maisha ya wananchi katika sekta zote, lakini kwenye maji nako kazi zinafanyika haswa.
Yaliyofanyika ni mengi kwenye maji, lakini makala hii inaangazia msamaha uliotolewa na Rais Dk. Samia kwa wadaiwa wa faini za ankara za maji ambao wamesitishiwa huduma ya maji kutokana na deni la faini.
Msamaha huo wa faini za maji umetangazwa Mei 08, 2025 bungeni na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kwa niaba ya Rais Dk. Samia wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 ambapo Shilingi Trilioni 1.01 zinatarajiwa kutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na matumizi mengine ya ofisi.
“Ninapenda kutoa salamu za Wizara kwa wananchi wote wenye faini kuwa Mama Samia Suluhu Hassan amesamehe faini hizo. Wafike katika Mamlaka za Maji kuanzia sasa hadi Mei 31, 2025, ili kupewa utaratibu wa kurejeshwa huduma za maji,” amesema Waziri Aweso.
Salamu hizi za upendo kutoka kwa Rais Dk. Samia kwa wananchi wake, ni habari njema sana kwani wapo baadhi ya wananchi ambao walishakata tamaa ya kurejeshwa huduma ya maji kutokana na faini walizotozwa kuwa kubwa na hivyo kutafuta njia mbadala za kupata maji, mathalani kuchota kwa majirani, mtoni, visimani ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Lakini sasa, kupitia maelekezo ya Rais Dk. Samia ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigania wananchi wake wapate huduma ya maji karibu na nyumba zao, anatoa hakikisho la kurejeshewa huduma ya maji kupitia msamaha wa faini za ankara za maji uliotangazwa, hivyo wananchi kuendelea kufurahia huduma hiyo muhimu katika maisha yao ya kila siku, ikizingatiwa kuwa “Maji ni Uhai.”
Huduma ya maji ni moja ya huduma muhimu ambayo kukosekana kwake kunaleta athari hasi za moja kwa moja na kuzorotesha juhudi za maendeleo zinazofanyika. Mathalani, matumizi ya muda mwingi katika kutafuta maji, kunaathiri shughuli za nyumbani, kiuchumi, ndoa, taaluma kwa wanafunzi na masuala mengine kadha wa kadha. Ni muhimu kuzingatia kuwa maji hayana mbadala wake, wananchi wakihitaji maji, basi wapelekewe maji.
Ili mwananchi aweze kunufaika na msamaha wa faini za ankara za maji uliotangazwa, anapaswa kutembelea ofisi ya Mamlaka ya Maji iliyopo katika wilaya yake ili kupata maelezo na namna ya kurejeshewa huduma ya maji.
SULUHISHO LA KUDUMU LA MADENI YA MAJI
Ili kuepukana na madeni sugu na faini za ankara za maji, Wizara ya Maji inapaswa kutenga fedha za kutosha na kutafuta fedha nyingine ili kuhakikisha wateja wote wa maji wanafungiwa mita za malipo kabla ya matumizi (pre-paid water meters). Hii itamaliza kabisa malimbikizo ya madeni na faini za ankara za maji kwa wateja wa maji. Kupitia mita hizi, mteja atanunua maji kabla hajayatumia, na pale kiwango cha maji alichonunua mteja kitakapokwisha, basi huduma ya maji itasitishwa, hivyo itamlazimu mteja kununua tena ndipo atakapopata huduma ya maji. Utaratibu huu unatumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia mfumo wake wa LUKU (Lipa Umeme Kadri Unavyotumia).
Wananchi wenye madeni yatokanayo na faini za ankara za maji changamkieni ofa hii ya aina yake iliyotolewa na mdau namba moja wa maji nchini – Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kabla ya Mei 31, 2025, na fedha ilivyokuwa ilipe faini, mwananchi anaweza kuitimia katika mipango yake mengine ya maendeleo. Ndiyo maana nasema hivi: Msamaha wa faini za ankara za maji uliotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umekonga nyoyo za wananchi hasa wa kipato cha chini waliokuwa na madeni makubwa yatokanayo na faini za ankara za maji.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.