Mbunge wa Jimbo la Madaba Mkoani Ruvuma, Dkt. Joseph Kizito Mhagama, amepata pongezi kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Uss, kwa kazi nzuri na ya kujituma anayoifanya katika kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza leo katika Shule ya Msingi Mkwera, Kata ya Lituta, mara baada ya kuanza ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Madaba, Ismail alisema kuwa Dkt. Mhagama ameendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa namna anavyowasilisha na kusimamia masuala ya wananchi bungeni.
Katika hotuba yake, Ismail alieleza kuwa mchango wa Dkt. Mhagama katika maendeleo ya jimbo lake unaonekana wazi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. Alisema kuwa dhamira ya dhati ya Mbunge huyo katika kuboresha maisha ya wananchi wake ni ishara ya uongozi wa kizalendo na unaojali maslahi ya wananchi.
Mbali na pongezi hizo, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alitoa wito kwa wananchi wa Jimbo la Madaba kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Alisisitiza kuwa uaminifu na mshikamano wa wananchi ndio msingi wa kuendeleza kasi ya maendeleo yaliyoanzishwa.
Wananchi wa Madaba nao wameonesha furaha na kuunga mkono kauli hiyo, wakieleza kuwa Dkt. Mhagama amekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo, hasa katika sekta za afya, elimu na miundombinu. Walisema wako tayari kuendelea kushirikiana naye na kumuunga mkono katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo endelevu.
Mwenge wa Uhuru kwa sasa uko Mkoani Ruvuma, ukitokea Mkoani Njombe. Unatarajiwa kukimbizwa katika Halmashauri zote nane za Mkoa huo, ambapo utakagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 76 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 95. Tayari Mwenge huo umekagua miradi 10 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1 katika Halmashauri ya Madaba.