Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera na pia Mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Fedha na Mipango UWT Taifa, Bi. Samira Khalfan, ameadhimisha Siku ya Mama Duniani kwa kuwatembelea wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Kabindi, wilayani Biharamulo. Ziara hiyo ililenga kuonyesha upendo, mshikamano na kuwapa faraja wanafunzi hao kwa kusherehekea siku hiyo maalum pamoja nao, leo tarehe 11 Mei 2025.
Katika maadhimisho hayo, Bi. Samira aliungana na walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo kukata na kula keki, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Siku ya Mama Duniani kwa njia ya kipekee. Tukio hilo lilileta furaha kubwa kwa wanafunzi hao ambao mara nyingi hujikuta wakikosa kushiriki katika matukio ya kijamii kama hayo.
Akiwa shuleni hapo, Bi. Samira alitoa msaada wa matenki makubwa ya kuhifadhia maji, ili kusaidia shule hiyo kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi. Alieleza kuwa maji ni hitaji muhimu kwa mazingira bora ya kujifunzia, hasa kwa watoto wenye mahitaji maalum ambao huhitaji huduma za kiafya kwa ukaribu zaidi.
Pamoja na msaada huo, alimpongeza Mhe. Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamuro Magharibi ambaye tayari ameshatoa msaada wa Magodoro 50 ambapo amemuunga mkono kwa kukabidhi mashuka 30 kwa ajili ya wanafunzi wanaolala katika mabweni ya shule hiyo ambayo yatasaidia kuboresha hali ya usafi na kuwafanya wanafunzi kujisikia kustarehe na kujihisi kuthaminiwa kama watoto wengine.
Bi. Samira pia alitoa motisha ya shilingi 400,000 kwa walimu wa shule hiyo kama ishara ya kutambua na kupongeza kazi kubwa wanayofanya ya kuwalea na kuwafundisha watoto wenye mahitaji maalum kwa moyo wa kujitolea. Alisisitiza kuwa walimu wa kundi hili wanastahili kutunzwa na kupewa motisha zaidi.
Katika hotuba yake kwa wanafunzi, walimu na wazazi waliohudhuria, Bi. Samira alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwajali watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwapa upendo, msaada na mazingira bora ya kujifunza. Alieleza kuwa kila mtoto ana haki ya kufurahia maisha na kupata elimu bora, bila kujali changamoto zake za kiafya au kimaumbile.