Songea_Ruvuma.
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, ametangaza rasmi kuanzishwa kwa mashindano ya Ndumbaro Cup yatakayofanyika hivi karibuni ili kuwahamasisha vijana kushiriki michezo na kuibua vipaji.
Tangazo hilo limetolewa leo Mei 12, 2025, katika hafla ya kugawa vifaa vya michezo kwa matawi ya CCM, ambapo Ndumbaro amekabidhi mipira 96 na seti 96 za jezi kwa maandalizi ya mashindano hayo.
Amesema kuwa Ndumbaro Cup ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, inayosisitiza umuhimu wa michezo kwa maendeleo ya vijana. “Kupitia michezo, vijana hujifunza nidhamu, kujituma, na kushirikiana. Pia tunawapa nafasi ya kuonekana na kuunganishwa na timu kubwa nchini,” alieleza.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha matumaini kwa vijana wa Songea Mjini, si tu katika sekta ya michezo bali pia katika kujenga afya, mshikamano na fursa za ajira.
Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa michezo ni nguzo muhimu ya kuimarisha amani na utulivu katika jamii, na kwa kupitia Ndumbaro Cup, Songea Mjini itaona mabadiliko chanya kwa vijana na jamii nzima.